Mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Uganda Dkt. Kizza Besigye na msaidizi wake Hajj Obeid Lutale wamerudishwa gerezani. / Picha  kwa hisani ya  Kampala Post.

Mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Uganda Dkt. Kizza Besigye na msaidizi wake Hajj Obeid Lutale wamerudishwa katika gereza la Luzira chini ya ulinzi mkali baada ya kusikilizwa kwa ombi lao katika Mahakama Kuu mjini Kampala.

Besigye na msaidizi wake, Hajj Obeid Lutale, walifikishwa katika Mahakama Kuu Kampala kwa ajili ya kusikilizwa kwa ombi la kutaka waachiliwe.

Kesi hiyo mbele ya Jaji Douglas Singiza, ilitokana na ombi lililowasilishwa na wanasheria wa Besigye Februari 5, la kutaka maelezo kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna Mkuu wa Magereza kuhusu kuendelea kuzuiliwa kwa mwanasiasa huyo.

Jaji Singiza alieleza wasiwasi kuhusu hali ya afya ya Besigye, akisema kwamba hangeweza kuendelea huku mgonjwa akiendelea kuwepo mahakamani.

"Ikiwa mfungwa ni mgonjwa, siwezi kuendelea na kesi. Anaweza kuzimia,” alisema jaji Singiza.

Besigye amekuwa katika mgomo wa kula huku akilalamika kucheleweshwa kwa kesi yake.

Hakimu aliamuru Besigye na Lutale warudishwe gerezani badala ya kubaki mahakamani.

Besigye na Obeid wamekuwa rumande tangu Novemba 2024 baada ya kutekwa nyara wakiwa jijini Nairobi nchini Kenya.

Baadaye walishtakiwa kwa makosa yanayohusiana na usalama na uhaini katika Mahakama Kuu ya kijeshi ya Uganda.

Hata hivyo, katika uamuzi wa mwezi uliopita, Mahakama ya Juu ilisitisha kesi ya raia katika mahakama za kijeshi.

Lakini Rais Yoweri Museveni katika taarifa yake, aliitetea serikali kwa kusema kuwa uendeshaji wa kesi hiyo umechelewa baada ya Mahakama ya juu kuamua kuhamisha kesi hiyo kutoka Mahakama ya Kijeshi na kuipeleka Mahakama ya Kiraia, mchakato unaochukua muda mrefu.

Mahakama Kuu inatarajiwa kutoa uamuzi wa ombi la wawili hao kuhusu kuachiwa kwa dhamana katika siku zijazo.

Wakati huo huo, mashirika ya kutetea haki za binadamu, wanasiasa wa upinzani na viongozi wa kidini wanataka Besigye aachiliwe mara moja.

TRT Afrika