Mkimbiaji wa mbio ndefu kutoka Kenya Sarah Chepchirchir amepigwa marufuku ya miaka nane  / Photo: Reuters

Safari ya michezo ya mkimbiaji wa mbio ndefu kutoka Kenya Sarah Chepchirchir imesimamishwa kwa muda baada ya kupigwa marufuku ya kutoshiriki katika michezo kwa muda wa miaka nane.

Chepchirchir ni mshindi wa zamani wa Tokyo Marathon.

Amepigwa marufuku na Shirika la World Athletics ambalo limeanzisha kitengo cha uadilifu cha riadha (Athletics Integrity Unit, AIU) ambacho jukumu lake ni kulinda uadilifu wa mchezo wa riadha,

Shirika hili linasema katika taarifa kuwa, mnamo tarehe 5 Novemba 2023, Mwanariadha huyo wa miaka 39 alitoa sampuli ya mkojo huko Chonburi, nchini Thailand, na uchunguzi wa sampuli ya maabara uliidhinishwa na Wakala wa Dunia wa Kupambana na Dawa za Kulevya (“WADA”) Bangkok, Thailand.

"Uchunguzi ulionyesha uwepo wa dawa ya " Testosterone," dawa Iliyopigwa marufuku chini ya Orodha ya WADA 2023...ni dawa iliyopigwa marufuku wakati wote," Athletics Integrity Unit imesema katika taarifa.

"Kwa hivyo, tarehe 22 Disemba 2023, AIU ilimpa mwanariadha notisi ya madai ya Sheria ya Kupambana na Dawa za Kulevya, ukiukaji na kusimamishwa kwa muda," imeongezea kuwa mwanariadha huyo alitarajiwa kutoa maelezo ya kina yaliyoandikwa baada ya tarehe 5 Januari 2024.

Lakini hakujibu, hata baada ya kupewa nafasi nyengine tena mara mbili.

Si mara ya kwanza kwa Chepchirchir kupatikana na hatia.

"Huu ni ukiukaji wa pili wa ....hapo awali ametumikia kipindi cha kutostahiki kwa miaka minne (4) kuanzia tarehe 6 Februari 2019. Hadi tarehe 5 Februari 2023 kwa Ukiukaji wa Sheria ya Kupambana na Matumizi ya Madawa ya Kulevya," kitengo hicho kimesema.

TRT Afrika