Uwezekano wa Rais William Ruto na mpinzani wake mkuu Raila Odinga kushirikiana serikalini ulionekana kutowezekana kwa wengi, lakini baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliona hilo.
Katika juhudi za kuleta utulivu katika utawala wake unaopigwa vita, Ruto aliteua viongozi wanne mashuhuri wa upinzani kutoka kambi ya Odinga kwenye baraza lake la mawaziri Jumatano iliyopita.
Wagombea wapya wa baraza la mawaziri wanaoungwa mkono na upinzani ni John Mbadi (Waziri wa Fedha), James Opiyo Wandayi (Waziri wa Nishati na Petroli), Hassan Ali Joho (Waziri wa Madini na Uchumi Buluu) na Wycliffe Oparanya (Waziri wa Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogo Ndogo).
Prof. Macharia Munene, mhadhiri wa historia katika Chuo Kikuu cha United States Internationl University-Afrika, alisema muungano huo haukushangaza bali uliharakishwa na mtikiso za Gen-Z.
"Ni mkakati wa kujinusuru kisiasa ambao utampa rais nafasi ya kufanya maamuzi kabla ya kuamua nini kitafuata baada ya hapo. Hii itategemea jinsi wabunge watakavyofanya katika kipindi cha wiki mbili au zaidi zijazo, wanapofanya kazi yao ya kuwachuja walioteuliwa. " Munene anaiambia TRT Afrika.
Kilichoanza kama hisia za kupinga kuongezeka kwa kodi ziligeuka kuwa wiki za maandamano yenye vurugu, na kusababisha vifo vya watu 50 na uharibifu mkubwa wa mali.
"Upinzani ungetaka sana kuwa uso wa msukumo huo, lakini hawakuwa na uhusiano wowote nayo, wakati huu," Munene anasema.
Anaamini matukio ya hivi majuzi nchini Kenya yaliweka upinzani katika eneo wasilolifhamu.
"Wanatamani wangekuwa ni wao wamechukua sifa kwa maandamano hayo. Sasa, inabidi watafute njia za kuondoa umaarufu kutoka kwa Gen-Zs," Munene anaongeza.
Je, upinzani ulimezwa?
Huku chama kikubwa cha upinzani kikishirikishwa serikalini, swali la msingi linabaki kuwa, ni nani atakayeikosoa serikali?
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaamini baada ya maandamano ya hivi majuzi, kutakuwa na umakini katika siasa na utawala wa Kenya, kukiwa na au bila chama mahiri cha siasa cha upinzani.
"Gen-Z ilionyesha njia ya kuweka serikali katika udhibiti," Munene anabainisha, akiongeza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kuibua wasiwasi wakati mambo yanaenda kombo. Wabunge, wawe wa upinzani au wa chama tawala, wanachaguliwa kuwakilisha wananchi, na sio serikali, Munene anasisitiza.
“Kwa hiyo pale wabunge wanaposhindwa katika wajibu wao wa kusimamia maslahi ya wananchi, basi wananchi wana haki ya kutekeleza agizo hilo na Wana-Z wamekuwa wakifanya hivyo, hadi tabaka la kisiasa likaingiwa wasiwasi mkubwa kwa sababu, wanapoteza mamlaka kwa watu ambao hawajachaguliwa," Munene anasema.
Kwa maisha ya kisiasa, kusitishwa kwa chuki ikawa ni muhimu. "Lazima watafute njia ya kutatiza harakati hii."
Sasa kwa vile serikali ya Kenya na upande mkubwa wa upinzani wako upande mmoja, je, hoja zinazotolewa na vijana zitapata majibu sahihi?
"Mtu angesema mvutano ungepoa kidogo, lakini itakuwa ni makosa kudhani kwamba yameisha, kwa sababu ikiwa masuala hayatashughulikiwa, basi kutakuwa na sababu ya watu kuendelea (na msukosuko)," Munene anabainisha.
Macho yaelekezwa bunge
Wabunge watakuwa chini ya uangalizi mkali wakati huu huku wakiwakagua wateule wapya wa baraza la mawaziri.
Baada ya mjadala wa Juni 25, ambapo bunge lilizidiwa na waandamanaji waliokuwa na hasira muda mfupi baada ya kupitisha mswada wenye utata wa kuidhinisha msururu wa nyongeza ya kodi, wachambuzi wanaamini wabunge sasa watakuwa wakijaribu kuthibitisha kuwa wanaweza kutegemewa.
"Bunge linajaribiwa tena," Macharia anaongeza: "Ikiwa wao (wabunge) wataonyesha kuwa wao ni chapa tu, basi inaweza kuwa sababu nzuri ya kurejea kwa kasi ya kusema 'hapana, hii haiwezi kuwa."
Wiki mbili zijazo, anasema, zinaweza kuwa muhimu kwa kile kitakachotokea.
Maadui rafiki wa kisiasa
Uhusiano wa Rais Ruto na kiongozi wa upinzani Odinga ni ufafanuzi kamili wa kali lakini tamu.
Walikuwa washirika wa karibu wa kisiasa kwa miaka mingi huku Ruto akiwa mfuasi mkuu ugombeanaji wa Odinga kuwa rais wa Kenya wakati wa uchaguzi wa 2007.
Baada ya uchaguzi huo, mgombea wa upinzani wakati huo Odinga, alikataa matokeo ya uchaguzi wa urais ambayo yalimpa ushindi Rais wa sasa Mwai Kibaki.
Na ghasia za baada ya uchaguzi zilizuka na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1000.
Mazungumzo ya kimataifa yalifikia kilele kwa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ambayo Ruto na Odinga waliungana huku Odinga akiwa waziri mkuu.
Hata hivyo, uhusiano kati ya wanasiasa hao wawili ulianza kudorora baada ya, mwaka wa 2010, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kumfungulia mashtaka William Ruto pamoja na wanasiasa wengine kadhaa wa Kenya kufuatia ghasia mbaya zilizotokea. Odinga hakuwa miongoni mwa walioshtakiwa.
Mnamo 2013, Ruto aliungana na mgombea urais wa upinzani Uhuru Kenyatta, ambaye pia alikuwa akikabiliana na mashtaka ya ICC. Baadaye ICC ilitupilia mbali mashtaka dhidi ya Ruto na Uhuru.
Baada ya Uhuru kumshinda Odinga katika uchaguzi huo, alimchagua Ruto kuwa makamu wa rais.
Kenyatta, hata hivyo, baadaye alimwalika Odinga kwa serikali yake, jambo ambalo lilimkasirisha naibu wa rais Ruto.
Ruto aligombea uchaguzi wa urais wa 2022 kinyume na matakwa ya bosi wake, Uhuru, ambaye alikuwa akiunga mkono azma ya Odinga ya urais.
Ruto, ambaye familia yake haikuwa na historia ya kisiasa ya kitaifa, aliapa kukomesha ''familia za kisiasa'' za Kenya, akimaanisha familia za Uhuru na Odinga, ambazo zina mizizi mikali ya kisiasa.
Alimshinda Odinga kwa kura kidogo katika uchaguzi wa urais wa Agosti 9, 2022. Tangu wakati huo, walikuwa maadui wakali wa kisiasa.
Uhusiano wa mihemko ya kisiasa hata hivyo umejirudia katika mduara kamili na hatua ya hivi punde ya Rais Ruto ya kutoa nyadhifa za uwaziri kwa wanasiasa wa Odinga.