Rais Joe Biden, ambaye aliwasili Angola Desemba 2, 2024 kwa ziara ya siku tatu, alisema anajivunia kuwa rais wa kwanza wa Marekani kuzuru taifa hilo la Afrika. / Picha: Reuters

Rais wa Marekani Joe Biden siku ya Jumanne alisema "mustakbali wa dunia uko barani Afrika" alipokutana na mwenzake wa Angola Joao Lourenco katika ikulu ya rais katika mji mkuu wa taifa hilo la Kusini mwa Afrika Luanda.

Biden, ambaye aliwasili Angola siku ya Jumatatu kwa ziara ya siku tatu, alisema anajivunia kuwa rais wa kwanza wa Marekani kuzuru taifa hilo la Afrika.

"Marekani yote iko katika Afrika na nadhani ushuhuda wa hilo... utawala wangu pekee umewekeza zaidi ya dola bilioni 3 nchini Angola ndiyo maana mustakabali wa dunia uko hapa, barani Afrika, Angola," alisema.

Biden, ambaye awali alikutana na Rais Ulisses Correia e Silva huko Sal, Cape Verde, nchi ya visiwa vya Afrika Magharibi, alisema ana nia ya kujadiliana na Angola jinsi demokrasia inavyoleta matokeo kwa watu.

Mwamko mpya

Alisema anajivunia sana kile Marekani na Angola zimefanya pamoja kubadilisha ushirikiano wa pande mbili.

Akitoa mfano wa njia ya reli inayoungwa mkono na Marekani, mradi muhimu wa miundombinu, uwekezaji katika nishati ya jua na kuboresha uhusiano wa intaneti, Biden alisema matokeo ya uhusiano kati ya Marekani na Angola yanajieleza yenyewe.

Lourenco, ambaye alielezea ziara ya Biden kuwa hatua ya mabadiliko, alitoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano katika sekta ya ulinzi na usalama kati ya Angola na Marekani, pamoja na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi ili kuongeza uzalishaji wa nishati.

Nchini Angola, njia ya reli inayoungwa mkono na Marekani, mradi muhimu wa miundombinu katika masuala ya uhusiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili, umeangaziwa.

Kupambana na China

Mradi huu unaunganisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia yenye rasilimali nyingi na bandari ya Angola ya Lobito kwenye Bahari ya Atlantiki.

Mtandao wa reli wa kilomita 1,300 (maili 800) kutoka Lobito hadi Congo unatarajiwa kutoa njia ya haraka ya kusafirisha bidhaa nje ya nchi kwenda Magharibi.

Mradi huo wenye thamani ya dola bilioni 1, uwekezaji mkubwa zaidi wa reli na Marekani barani Afrika, unaweza kukabiliana na mnaso wa China kwenye madini muhimu kama vile shaba na kobalti kutoka Congo, kulingana na wachambuzi.

Biden ameratibiwa kuzuru jumba la makumbusho la utumwa la Angola katika mji mkuu Luanda na kusimama katika bandari ya Lobito siku ya Jumatano.

TRT Afrika