Shughuli ya kuhesabu kura inaendelea nchini Msumbiji baada ya mamilioni kupiga kura katika uchaguzi wa Jumatano wa rais na wabunge.
Kujumlisha kura kulianza muda mfupi baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa saa kumi na mbili jioni kwa saa za ndani ( 1600 GMT), huku matokeo ya awali yakitarajiwa baada ya takriban wiki mbili.
Rais anayemaliza muda wake Filipe Nyusi, 65, ambaye anajiuzulu baada ya ukomo wa mihula miwili, alitoa wito kwa wananchi wake kuendelea kuwa watulivu na wavumilivu baada ya siku nzima ya kupiga kura bila kuripotiwa matukio makubwa.
“Pia ningeomba kusiwe na kundi la wananchi linalosumbua au kutishia wengine, kila kitu kifanyike kwa amani na utulivu na tuepuke kutangaza matokeo kabla ya wakati,” alisema Nyusi.
Matatizo ya udanganyifu
Viongozi wawili wakuu wa upinzani tayari wameonya dhidi ya udanganyifu katika uchaguzi katika taifa hilo la kusini mwa Afrika linalokumbwa na makundi ya wapiganaji kaskazini mwa nchi hiyo.
Baada ya kupiga kura yake, mgombea wa upinzani Venancio Mondlane alikosoa mchakato huo.
Uchaguzi uliopita wa urais, mwaka 2019, ambao Frelimo ilishinda kwa asilimia 73 ya kura, ulikumbwa na dosari, huku uchaguzi wa manispaa wa 2023 uliishia kwa vurugu baada ya matokeo kupingwa na upinzani.
"Mabadiliko" ndio yalikuwa gumzo midomoni mwa wapiga kura wengi, lakini wachambuzi walisema wanatilia shaka uchaguzi huo ungeleta mengi. Hakuna kitakachobadilika," alisema Domingos Do Rosario, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Eduardo Mondlane cha Maputo, akizungumzia taasisi dhaifu na majadiliano ya kisiasa.
Ushiriki katika uchaguzi uliopita wa urais ulikuwa karibu asilimia 50 ya waliojisajili.
Waangalizi walisema idadi ya wapiga kura inaweza kuongezeka mwaka huu, ingawa hakuna idadi rasmi iliyotolewa. Mbali na rais mpya, raia wa Msumbiji wanawapigia kura magavana 10 na wabunge 250.
Mabadiliko ya kizazi
Mgombea wa FRELIMO kuchukua nafasi ya Nyusi ni gavana wa jimbo ambaye sio maarufu, Daniel Chapo mwenye umri wa miaka 47, ambaye pia alitoa wito wa utulivu baada ya kupiga kura yake.
Kuchaguliwa kwake kungeashiria mabadiliko makubwa: angekuwa rais wa kwanza wa Msumbiji aliyezaliwa baada ya uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1975 na wa kwanza kutopigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 16 kati ya FRELIMO na RENAMO.
Wagombea wengine wawili ni Ossufo Momade, 63, wa Renamo, na Lutero Simango, 64, wa Mozambique Democratic Movement.
Simango pia ni mkosoaji mkubwa wa Frelimo, ambao viongozi wake anawataja kama "wezi waliovaa nguo nyekundu", ambayo ni rangi ya chama.
Baada ya kupiga kura yake, Momade alitoa wito wa "uamuzi wa watu kuheshimiwa." Zaidi ya asilimia 74 ya wakazi wa Msumbiji waliishi katika umaskini mwaka 2023, kulingana na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Uwekezaji wa gesi
Nchi hiyo ilikuwa na matumaini ya kuimarika kwa uchumi kutokana na ugunduzi wa mwaka 2010 wa hifadhi kubwa za gesi kaskazini, lakini ghasia za waasi katika jimbo la Cabo Delga do zilisababisha ExxonMobil na TotalEnergies kusimamisha miradi yao.
Uchumi utahitaji kuwa kipaumbele kwa serikali, alisema Aleix Montana, mchambuzi katika shirika la ushauri la Verisk Maplecroft lenye makao yake makuu nchini Uingereza.
"Rais mpya wa Msumbiji atalazimika kukabiliana na viwango vya juu vya deni la taifa na ukusanyaji dhaifu wa mapato, wakati miradi muhimu ya nishati inaendelea kucheleweshwa kutokana na uasi huko Cabo Delgado," alisema.