Venancio Mondlane anadai kuwa "ushindi" wake katika uchaguzi wa rais wa Oktoba 2024 nchini Msumbiji uliibiwa. / Picha: Reuters

Kiongozi wa upinzani wa Msumbiji ambaye ameongoza zaidi ya miezi miwili ya maandamano dhidi ya matokeo ya uchaguzi yenye utata kutoka nje ya nchi hiyo ametangaza Jumapili kuwa atarejea kabla ya kuapishwa kwa rais mpya.

Venancio Mondlane, ambaye aliondoka nchini baada ya wakili wake kupigwa risasi Oktoba 19, alisema katika matangazo ya moja kwa moja kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook kwamba atawasili katika uwanja wa ndege wa Maputo wa Mavalane siku ya Alhamisi.

Akiwa uhamishoni katika eneo lisilojulikana, ameitisha maandamano kupinga matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 9.

Maandamano hayo yamesababisha vifo vya takriban watu 300, kulingana na takwimu za shirika la haki za mitaa.

Matokeo yaliyothibitishwa na Mahakama Kuu yalisema Mondlane alipata 24% ya kura za urais ikilinganishwa na 65% ya mgombea urais wa chama tawala cha FRELIMO Daniel Chapo.

Siku ya kuapishwa

Chapo, 47, anatazamiwa kuapishwa Januari 15, akichukua nafasi ya Rais Filipe Nyusi baada ya kumaliza mihula miwili.

Mondlane anasisitiza kuwa uchaguzi uliibiwa na kwamba hesabu nyingine ilisema yeye ndiye mshindi. Misheni kadhaa za waangalizi wa kimataifa pia zimesema kulikuwa na makosa.

"Kama wanataka kuniua. Wakitaka kunikamata nikamateni. Najua kwamba nikiuawa, hasira ya watu wengi itakayosikika nchini Msumbiji haitakua na mfano katika historia ya Afrika na Msumbiji." Mondlane alisema.

'Alhamisi saa mbili asubuhi'

"Ikiwa ni kwa sababu yangu, ikiwa ni kwa sababu ya Venancio, basi Venancio atakuwa siku ya Alhamisi, saa mbili asubuhi, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mavalane," alisema.

Chama cha FRELIMO kimetawala nchi hiyo tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ureno mwaka 1975.

AA