Collins Jumaisi mshukiwa mkuu nchini Kenya katika mauaji ya mfululizo ambapo miili iligunduliwa katika eneo la taka la Kware katika mitaa ya Mabanda ya Mukuru, amefikishwa mahakamani.
Collins Jumaisi akifikishwa katika mahakama za Kiambu mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi Peter Ooko. Hata hivyo, hakimu wa mahakama hiyo alikataa kusikiliza kesi hiyo kwa madai kuwa, mahakama ya Kiambu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Hakimu alihamisha kesi hiyo hadi katika mahakama ya sheria ya Makadara ambapo mshukiwa atafikishwa mahakamani chini ya maombi mengineyo huku polisi wakitafuta muda zaidi wa kukamilisha upelelezi.
"Mshukiwa alikiri kuwashawishi, na kuwauwa wanawake 42 kutoka 2022 na ya hivi karibuni zaidi ya Alhamisi iliyopita, Julai 11. Mshukiwa alidai muathiriwa wake wa kwanza alikuwa mke wake ambaye alimnyonga hadi kufa kabla ya kuukata mwili wake," mkuu wa kitengo cha makosa ya jinai, Mohamed Amin alisema Jumatatu.
"Kutokana na kuhojiwa kwetu, waathiriwa wake wote wameuawa kwa mtindo huo huo. Uchunguzi wetu bado unaendelea," Amin aliongezea katika taarifa kwa wandishi wa habari.
Mshukiwa akana mauaji
Hata hivyo Khalusha, kupitia kwa wakili wake John Maina Ndegwa, alidai aliteswa na kulazimishwa kukiri kuwa aliwaua wanawake hao. Wakili huyo aliiomba mahakama kumruhusu kupata huduma ya matibabu.
"Mteja wangu, akiwa amekaa hapo, anahitaji matibabu ya haraka, kwa sababu katika kipindi hicho aliwekwa kizuizini, alinyanyaswa, kuteswa, jambo la kuwa amekiri kuhusika katika mauaji ya watu 42 kama walivyoambiwa wananchi ni la kuchekesha,” alidai Ndegwa mbele ya Mahakama ya Sheria ya Makadara.
Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) hata hivyo ilipuuzilia mbali madai hayo ya unyanyasaji, ikibaini kuwa ni afisa mmoja tu wa polisi aliyepewa mshukiwa kurekodi taarifa yake.
DCI ilitaka Khalusha azuiliwe kwa siku 30 hadi kukamilika kwa uchunguzi wa mauaji hayo, ikisema iwapo ataachiliwa kuna uwezekano wa kuendelea na shughuli za uhalifu.
Hakimu Mkuu Irene Gichobi hata hivyo aliruhusu DCI kumzuilia mshukiwa katika kituo chochote cha polisi kwa siku 30 alizoomba ili kukamilisha uchunguzi.
Mama wa mke wa Colins aliyedai kumuuwa ametoa taarifa yake kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), akielezea jinsi binti yake alivyopotea tangu 2022.
"Mnamo 2022, namba yake ya WhatsApp ilizima, na hatujawahi kusikia kutoka kwake," mama huyo alisema.
Polisi pia walisema walipata vitu vingi kutoka kwa nyumba ya mshukiwa ikiwa ni pamoja na simu za mkononi, mkoba na nguo za ndani za kike ambazo zitatumika kama ushahidi.