Hospitali imelazimika kutafuta wauguzi zaidi kutoka hospitali za karibu kumudu ongezeko la wagonjwa Picha: idara ya afya Gauteng 

Mlipuko mpya wa kipindupindu, katika mkoa ulio na watu wengi zaidi nchini Afrika Kusini, Gauteng umefikia 12 mpaka siku ya Jumatatu, kwa mujibu wa idara ya afya ya mkoa huo.

Miongoni mwa waathiriwa ni mtoto wa miaka mitatu, huku watu wengine 37 wakilazwa hospitalini katika hali mahututi, msemaji wa idara hiyo ameambia TRT Afrika.

Mlipuko wa mwisho wa kipindupindu nchini Afrika Kusini ulikuwa 2009 ambapo zaidi ya maambukizi 12,000 yaliripotiwa baada mlipuko kutokea nchi jirani Zimbabwe.

Idara ya afya ya Gauteng imesema kuwa watu 95 kutoka kitongoji cha Hammanskraal, kaskazini mwa mjimkuu, Pretoria, wamefika hospitalini katika wiki moja iliyopita wakiwa na dalili za ugonjwa huo. Uchunguzi wa kiafya umethibitisha 19 kati yao walikuwa na kipindupindu.

Ugonjwa huo husambazwa kwa maji machafu na husababisha kuharisha. Walioambukizwa wanaweza kufariki katika muda mfupi wasipo pokea matibabu.

Wakaazi wa eneo hilo wamehimizwa kutokunywa maji ya bomba huku tanki zikitumiwa kusambaza maji.

Vyumba viwili zaidi vimetengwa kwa ajili ya kuwapoakea wagonjwa, na wauguzi kuongezwa kutoka hospitali za karibu ili kumudu ongezeko la wagonjwa.

TRT Afrika