Huduma ya Polisi ya Kitaifa Kenya (NPS) imefafanua kuwa kuondolewa ghafla maafisa wa usalama wa Jaji Lawrence Mugambi, kulikuwa chini ya uamuzi wa inspekta jenerali wa polisi.
Hii inakuja siku chache baada ya Jaji huyo kumhukumu kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli kifungo cha miezi sita gerezani.
Alihukumiwa kwa kukosa kufika mahakamani mara saba licha ya kwa wito wa jaji.
Katika taarifa yake Masengeli alisema kuwa aliwahamisha maafisa hao wawili "kwa madhumuni ya kuhudhuria mafunzo ya usalama za VIP" na kwamba mipango ifaayo ilifanywa kumudu usalama wa Jaji Mugambi.
Taarifa ya kaimu mkuu huyo wa polisi inafuata malalamiko kutoka kwa jaji mkuu Martha Koome kwamba maafisa wa usalanma wa jaji Mugambi waliondolewa wikendi baada ya kupokonywa silaha.
"Hatua za kulipiza kisasi dhidi ya maafisa wa mahakama hazifai. Tume ya huduma ya sheria inatoa wito kwa polisi wa taifa kurejesha usalama wa Jaji Mugambi,” Martha Koome alisema katika taarifa aliyotoa Jumatatu.
Kaimu Mkuu wa polisi hata hivyo amesisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria, Rais, Naibu Rais na Rais Mstaafu ndio pekee wanastahili kupata maafisa binafsi wa usalama.
"Watu wengine wanapewa usalama wa kibinafsi kulingana na vigezo vilivyowekwa hapo juu na, katika Sera, zilizoundwa na Huduma ya taifa ya Polisi na kama inavyoweza kuamuliwa na inspekta jenerali wa polisi mara kwa mara," alisema katika taarifa.
"Muda wa Majaji kwa kuzingatia hilo pekee haujumuishi usalama wa mtu binafsi kama suala la kisheria. Kwa mujibu wa Sera ya Watu Mashuhuri (VIP), VIP inalindwa na vitengo maalum ikiwa ni pamoja na Usalama wa Serikali." Maelezo yake yalisema.
Jaji mugambi katika hukumu yake alidai kuwa Masengeli alikuwa ameidharau mahakama kwa kukosa kuja mbele yake moja kwa moja,
Masengeli alitakiwa kuieleza Mahakama kuhusu madai ya kutekwa nyara kwa ndugu wawili na mwanaharakati mmoja, kwa kipindi cha wiki mbili.
Kaimu Inspekta huyo ameagizwa kufika mbele ya hakimu ana kwa ana kueleza ni kwa nini wanaume hao watatu waliotekwa nyara huko Kitengela, Nairobi hawajaachiwa hadi sasa.
Inadaiwa kuwa, ndugu wawili Jamil Longton, Aslam Longton na mwanaharakati Brian Njagi walichukuliwa kinguvu na watu waliovalia suti, wanaodaiwa kuwa maofisa wa Polisi kutoka Nairobi, huku wakishindwa kutoa sababu za kuwakamata.