Mkuu wa Mashtaka Uganda akataa kutoa kesi za raia kwa mahakama ya kijeshi

Mkuu wa Mashtaka Uganda akataa kutoa kesi za raia kwa mahakama ya kijeshi

Mahakama ya kijeshi nchini Uganda imekuwa ikisikiliza kesi ya raia hasa mara kwa mara wale wanaoshitakiwa.
Mwanasiasa mkongwe wa upinzani Kiiza Besigye na msaidizi wake Obeid Lutale wameshtakiwa katika mahakama ya Kijeshi tangu Disemba 2024/ Picha: Reuters

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Uganda imekataa mapendekezo ya baadhi ya wabunge kufikiria kuchukua kesi za raia wanaoshtakiwa kwenye Mahakama ya kijeshi.

Mkurugenzi wa Mashtaka Frances Abodo amesema katiba haimruhusu.

"Siwezi kuchukua kesi chini ya Mahakama ya kijeshi. Tumelitazama hilo nataka nibaki kwenye laini yangu ya kazi tu," Abodo alisema.

Abodo alitoa msimamo huo wakati alipofika mbele ya Kamati ya Sheria na Bunge, kuwasilisha pendekezo la Bajeti ya 2025/26 kwa Ofisi ya Kurugenzi ya Mashtaka.

"Mtanisamehe naweza nisitoe maoni kwenye hizo kesi maana swali linalofuata ni kwamba nitoe maoni yangu kwenye hizo kesi ...naweza kunukuliwa vibaya halafu kosa la kutoheshimu mahakama linipate, ” alisema Abodo.

Mwaka wa 2018 kiongozi wa chama cha upinzani cha NUP Robert Kyagulany, maarufu Bobi wine, alipelekwa katika mahakama ya kijeshi pamoja na wafuasi wake kadhaa/ Picha: AFP

Kauli hiyo ya Abodo ilitokea akijibu swali lililoulizwa na Asuman Basalirwa mbunge wa Manispaa ya Bugiri aliyempa changamoto kiongozi wa mashtaka kufikiria kuchukua kesi za raia wanaoshtakiwa katika Mahakama ya Kijeshi.

"Tuna maoni kwamba huku katiba katika kiungo kimoja inamruhusu DPP kuweza kufungua kesi katika mahakama zote isipokuwa Mahakama ya Kijeshi, inapokuja kuchukua kesi au kusitisha kesi za mahakama hiyo tuna maoni kwamba kwa kweli, Katiba inaweza kubali," Basalirwa alisema.

Kwa mfano kwa sasa mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Uganda Kiiza Besigye na msaidizi wake Obeid Lutale wana kesi mbele ya mahakama ya kijeshi wakishitakiwa tangu Disemba 2024 kwa kumiliki silaha na kuhusika na uhaini.

Mawakili wao wamekuwa wakilalamika kuwa wao si wanajeshi hivyo kesi yao ipelekwe katika mahakama ya kawaida.

Mwaka wa 2018 kiongozi wa chama cha upinzani cha NUP Robert Kyagulany, maarufu Bobi wine, alipelekwa katika mahakama ya kijeshi pamoja na wafuasi wake kadhaa. Walishtakiwa kwa uhaini lakini baadae wakaachiliwa.

TRT Afrika