Mkutano wa kimataifa uliofanyika mjini Paris, Ufaransa umetoa ahadi ya dola bilioni 2.1 kwa ajili ya kusaidia Sudan ambayo kwa sasa imeathiriwa na vita kwa mwaka mmoja. Nchi 58 zilihusika katika mkutano huu.
Vita nchini humo kati ya jeshi la Sudan na kikundi cha Rapid Support Forces vilianza 15 Aprili 2024 na sasa vinaingia mwaka wa pili.
"Mkutano huko Paris umesaidia kuzingatia kile ambacho kimesahaulika sana, na ingawa ni chanya kwamba nchi nyingi zimeonyesha nia ya kusaidia, euro bilioni 2 haitoshi kukidhi mahitaji makubwa na yanayokua ndani ya Sudan na nchi jirani. " Claire Nicolet, Afisa wa shirika la MSF Sudan amesema.
Umoja wa Mataifa ulitoa wito wa dola bilioni 4.1 kwa jumla, hivyo ahadi zilitolewa na nchi tofauti zimepunguza mahitaji haya kidogo.
Pesa hizo huenda zitasaidia kuongeza msaada wa kibinadamu katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Wanajeshi wa Sudan, lakini kwa kizuizi cha sasa cha usafirishaji wa vifaa na wafanyakazi katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa vikosi vya Rapid Support Forces, itamaanisha kuwa mamilioni ya watu watasalia bila msaada.
Wakati huo huo, Uingereza siku ya Jumatatu ilitangaza vikwazo dhidi ya biashara zinazohusishwa na pande zinazozozana nchini Sudan.
Wizara ya Mambo ya Nje Uingereza ilisema "hatua kali" zitajumuisha kufungia mali kwa kampuni zilizounganishwa na vikosi vya jeshi la Sudan na Rapid Support Forces.
Umoja wa Mataifa unasema vita nchini Sudan vinaonekana kusahaulika.
"Sehemu kubwa ya dunia imekuwa ikizingatia mzozo ambao ulitokana na Mashariki ya Kati. Kuhusu jinsi matukio hayo yalivyo, sehemu nyingine za dharura za maisha na kifo zinasukumwa kwenye kivuli (na kuwekwa pembeni)," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres aliwaambia waandishi wa habari baada ya Baraza la Usalama kukutana, Jumatatu.
"Dunia inasahau kuhusu watu wa Sudan," Guterres alisema.
Zaidi ya watu 14,000 wameuawa na takriban 33,000 wamejeruhiwa katika vita vya mwaka mzima.
Takriban watu milioni 9 wamelazimika kuyahama makazi yao ama kuelekea maeneo salama ndani ya Sudan au nchi jirani, kulingana na Umoja wa Mataifa.