Maisha ya mamilioni ya wananchi wa Sudan yamebaki katika hali ya taharuki katika kipindi cha nusu mwaka sasa tangu mapigano makali kati ya jeshi la Sudan na kikundi cha Rapid Response Forces vilipoanza mwezi Aprili, 15 mwaka huu.
Mapigano hayo yalizuka katika mji mkuu wa Khartoum na kusambaa katika miji mengine ya Darfur and Kordofan.
"Takriban watu 9,000 wameripotiwa kuuawa, huku zaidi ya milioni tano na laki sita wamefurushwa katika makazi yao hali inayofanya watu milioni 25 kuhitaji msaada." Umoja wa Mataifa umesema katika taarifa yake.
"Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kuwaacha watu wa Sudan," Martin Griffiths, ambae ni Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa, amesema, akitoa wito kwa suluhu kupatikana ili kumaliza vita nchini humo.
Jitihada za kusitisha vita hazijafaulu
Mwezi Septemba, 2023, Jenerali Abdel-Fattah Al-Burhan alisema kuwa hamu yake ilikuwa kutafuta suluhu ya kudumu na amani katika mgogoro huo wakati akihudhria mkutano wa viongozi wa Umoja wa Mataifa.
"Kila vita huishia na amani, iwe ni kupitia mazungumzo au nguvu. Tunaendelea na njia hizo mbili, na njia tunayopendelea ni njia ya mazungumzo," Al-Burhan alisema kando ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa UNGA, huko New York nchini Marekani.
Mwezi huu wa Oktoba, Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa liliamua kuanzisha ujumbe maalum kwa ajili ya Sudan.
Ujumbe huo utajumuisha wajumbe watatu wenye utaalamu katika sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu, watakaoteuliwa na rais wa Baraza la Haki za Kibinadamu.
Tayari jitihada za kutafuta suluhu katika mzozo huo unaoongozwa na majenerali wawili, hazijaonekana kufua dafu.
Muungano wa kikanda wa IGAD uliteuwa kamati ya kuongoza jitihada za amani ikiongozwa na rais wa Kenya William Ruto. Hata hivyo, uongozi wa Sudan ambao kinara wake ni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ulikataa Kenya kuongoza juhudi hizo.
Sura ya vita nchini Sudan inaonekana kwa wakimbizi ambao sasa wamekimbilia katika nchi jirani.
Takwimu zinaonyesha, mpaka sasa kuna zaidi ya wakimbizi 420,000 kutoka nchini Sudan huku zaidi ya laki tatu wakiwa Misri na wengine 19,000 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Wengine zaidi ya elfu 30,000 wamekimbilia nchini Ethiopia.