Na Dayo Yussuf
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Ngoma zinavuma katika kuadhimisha Jubilei ya Fedha ya Afrika Mashariki tarehe 30 Novemba.
Sherehe za mafanikio makubwa wakati kikundi cha wanachama wa nchi 8 kinaposonga ili kuunganisha rasilimali zake kwa uchumi ulio na nguvu zaidi na wazi.
Lakini hata kama eneo kubwa la Afrika Mashariki likijikagua ili kusonga mbele, kujitafakari kwa wanachama kunaleta maswali mengi unapochimba zaidi hadi ngazi ya raia.
‘’Kwa kweli tumepiga hatua katika kujenga uhusiano ikilinganishwa na miaka ya nyuma,’’ anasema mfanyabiashara wa Tanzania Hassan Omar.
"Kuondolewa kwa viza kwa wanachama kumetuwezesha wengi wetu kutembea kwa uhuru kati ya nchi na nchi na kupanua biashara yetu,’’ anaiambia TRT Afrika.
Lakini hata kwa uhuru uliotangazwa kutoka ngazi ya serikali, Hassan anahisi kuna vikwazo ambavyo vinarudisha nyuma watu wengi. ‘’Tunasema tunataka usawa kwetu sote lakini hatuko sawa. Viwango vya elimu ni tofauti, uchumi wetu hauko sawa na mengine mengi,’’ anasema Hassan.
‘’Dhana ya EAC haijaeleweka kwa baadhi ya watu wa eneo hili,’’ anasema Prof. Kenneth Simala, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro nchini Kenya.
‘’Watu hawawezi kuwa sawa, na ni ukosefu wa usawa ambao utangamano unastahili kuuponya. Ili kusaidia watu kufaidika kutoka kwa kila mmoja. Kuwafanya watu wahisi kama kuna jukumu na sio kunyonywa,’’ anaongeza Prof Simala.
Hivi majuzi wakati wa uzinduzi wa nembo ya ukumbusho wa jubilei ya fedha, Katibu Mkuu wa EAC Veronica Nduva alibainisha kuwa biashara ya ndani ya kanda imekua kwa kiasi kikubwa na kufikia Dola za Marekani bilioni 10.17 ifikapo Septemba 2022.
Ongezeko hili limechangiwa na uungwaji mkono mkubwa wa kisiasa miongoni mwa nchi wanachama.
EAC inasifu baadhi ya maendeleo makubwa katika kanda ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa usafirishaji huru wa watu, bidhaa, huduma na mitaji.
Aidha, EAC imepiga hatua kubwa katika kuanzisha Umoja wa Fedha wa Afrika Mashariki (EAMU), ikiwa na mipango ya kuanzisha sarafu moja ifikapo mwaka 2031.
Lakini hii haina maana yoyote ikiwa mwananchi wa kawaida hajionei au kuhisi mwenyewe moja kwa moja.
‘’Mambo ambayo nilifikiri yangeninufaisha ndani ya jumuiya, siyahisi. Bado hatuna mitaala inayofanana shuleni. Bado hatuzungumzi lugha moja na changamoto nyingine nyingi. Nafasi ya kisiasa katika nchi zote ni tofauti kabisa. Wengine wana uhuru fulani kama uhuru wa kujieleza ilhali katika nchi nyingine huwezi hata kuikosoa serikali yako,’’ analalamika Hassan.
Lakini Prof. Simala, ambaye aliwahi kufanya kazi kama Katibu Mtendaji wa Kiswahili katika EAC, anasema hii ni kwa sababu kuna mfarakano mkubwa kati ya wasomi wa kisiasa wanaoendesha EAC na watu halisi mashinani.
"Changamoto tuliyonayo ni kwamba utangamano wa EAC unaundwa kuanzia juu hadi chini. Raia wa Afrika Mashariki wanatakiwa kumiliki mchakato wa umoja. Kwa bahati mbaya EAC imekwama katika ngazi ya uongozi wa kisiasa. Limekuwa suala la kipekee la tabaka la kisiasa na si la wananchi.’’
Katika shamrashamra za sherehe, Jubilee ya Fedha itaadhimishwa na mkutano wa kilele wa wakuu wote wa nchi chini ya mada, "Kukuza Biashara, Maendeleo Endelevu, Amani na Usalama kwa Maisha Bora."
Kwa upande mwingine, jumuiya inaonekana kuegemea zaidi katika kukuza biashara. Wachambuzi wanasema inaweza kuwa kikwazo kwa jumuiya.
‘’Kuna juhudi moya za utangamano duniani kote. Lakini EAC imekwama katika ushirikiano wa kikanda wa zamani ambapo kila kitu kilijikita katika biashara na masoko. Lakini utangamano mpya huleta mambo mengine. Utangamano sio tu kuhusu biashara au masoko unapaswa kuwa kuhusu watu, na si lazima watu walio katika biashara, lakini watu wanaopenda utamaduni wa elimu na umoja,’’ Prof Simala anaiambia TRT Afrika.
Ndiyo, EAC imepata mafanikio makubwa katika baadhi ya maeneo na maendeleo haya yamefungua fursa za ajira, upatikanaji wa elimu na matarajio ya biashara kwa mamilioni ya watu wa Afrika Mashariki, huku sekta binafsi ikiibuka kuwa kichocheo kikuu cha ukuaji wa uchumi ndani ya EAC.
Lakini wataalamu wanaonya kwamba ikiwa haitafanywa kwa ushirikishwaji kamili wa wananchi mashinani, wanasiasa hawawezi kuaminiwa kuivukisha jumuiya hadi kutimia malengo yake peke yao.