Uchunguzi dhidi ya mshukiwa wa kiongozi wa madhehebu ya Kikisristu anayeshutumiwa kuwachochea wafuasi wake 428 kujiua kwa njaa, umetaja "kufeli" kwa mifumo ya usalama na uhalifu nchini Kenya, kulingana na ripoti iliyoonekana na shirika la habari la AFP.
Aliyejiita mchungaji Paul Nthenge Mackenzie amekuwa chini ya ulinzi wa polisi tangu katikati ya mwezi wa Aprili baada ya kupatikana kwa mabaki ya binadamu katika msitu wa Shakahola karibu na pwani ya Bahari ya Hindi.
Dereva wa teksi wa zamani na mwanzilishi wa Kanisa la Good News International anatuhumiwa kuwahubiria wafuasi wake wafe njaa “kumlaki Yesu”.
Japo njaa inaonekana kuwa sababu kuu ya vifo, baadhi ya wahasiriwa - ikiwa ni pamoja na watoto - walinyongwa, kupigwa au kuzibwa pumzi, kulingana na uchunguzi wa miili iliyofanywa na serikali.
Mashtaka kuondolewa
"Kenya imekumbwa na vifo vilivyohusishwa na misimamo mikali ya kidini hapo awali, hata hivyo, mkasa wa Shakahola umesajili idadi kubwa zaidi ya vifo katika historia iliyorekodiwa nchini Kenya," tume ya uchunguzi ya Seneti ilisema kwenye ripoti yake.
Iliongeza kuwa mchungaji huyo aliyejitangazia mwenyewe unabii alikabiliwa na mashtaka mwaka wa 2017 kwa mahubiri yake ya kupindukia, lakini "mfumo wa haki ya jinai ulishindwa kuzuia shughuli mbaya za Paul Mackenzie huko Shakahola".
Mackenzie aliachiliwa kwa makosa ya itikadi kali mwaka 2017 kwa kutoa mafundisho ya shule kinyume cha sheria - alikataa mfumo rasmi wa elimu ambao alidai hauendani na Biblia.
Polisi kushindwa
Tume ya uchunguzi pia ilitaja kushindwa kwa jeshi la polisi la eneo hilo, ambalo lilipokea "malalamiko ya mara kwa mara ya viongozi wa dini na jamii dhidi ya shughuli zake tangu mapema 2017".
Malalamiko hayo yalihusiana na upinzani wa Mackenzie dhidi ya elimu rasmi na matibabu, pamoja na "kuwafanya watu wazima kuwa na msimamo mkali kujiuzulu kazi zao na kujiunga na kanisa" na "kuwashikilia watu mateka".
Ripoti hiyo pia ililaumu "kutochukua hatua" kwa kamati ya usalama ya kaunti ya eneo hilo, ambayo "ilimwita Paul Mackenzie na kumuonya dhidi ya mafundisho yake ya itikadi kali na kuwaweka wafuasi katika mazingira ya kinyama".
Kudhibiti makanisa
Taifa lenye Wakristo wengi, Kenya imetatizika kudhibiti makanisa na madhehebu yasiyofaa ambayo yanajihusisha na uhalifu.
Kuna zaidi ya makanisa 4,000 yaliyosajiliwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki yenye watu milioni 53, kulingana na takwimu za serikali.
Tume hiyo ilikashifu sheria ya sasa kuwa "haifai" na kutaka bunge la nchi hiyo kupitisha "Mswada wa Mashirika ya Kidini" ili kutoa mfumo wa kisheria wa udhibiti wa taasisi za kidini.
Uchunguzi na utafutaji wa miili katika msitu wa Shakahola bado unaendelea.
Pindi utakapokamilika, Mackenzie na washtakiwa wenzake 29 watafunguliwa rasmi mashtaka, huku waendesha mashtaka wakitangaza mwezi Mei kwamba mchungaji huyo angekabiliwa na mashtaka ya ugaidi.