Hafla ya mazishi ya mwanariadha bingwa Kelvin Kiptum imeanza katika kijiji chake katika kaunti ya Uasin Ngishu.
Mazishi hayo yanahudhuriwa na rais wa Kenya William Ruto pamoja na viongozi wengine hasa katika sekta ya michezo kimataifa.
Hata hivyo, wakati mipango ya mazishi ya bingwa huyo ikiendelea, mwanamke mmoja ameripotiwa kwenda mahakamani kutaka mazishi yasitishwe akidai kuwa ni mama wa mtoto wa Kiptum. Hata hivyo, mahakama imekataa ombi hilo.
Siku ya Alhamisi, Mahakama Kuu mjini Eldoret, ilikataa kutoa agizo la kusitisha mazishi ya Kiptum baada ya mwanamke mwenye umri wa miaka 22 kuwasilisha kesi akidai kuwa ana mtoto wake.
Jaji Robert Wananda alitupilia mbali ombi lililowasilishwa na Edna Awuor Otieno. Jaji alisema kuwakuwa mazishi ya marehemu Kiptum ni ya manufaa ya umma.
"Mipango ya mazishi ya marehemu iko katika hatua ya juu, na kwa hivyo, kusimamisha kunaweza kuleta usumbufu kwa kuzingatia rasilimali ambazo zimewekwa katika maandalizi," alisema Jaji Wananda.
Kelvin Kiptum, alifariki kufuatia ajali ya barabarani katika barabara ya Eldoret-Kaptagat, mkoa wa Bonde la Ufa.
Kiptum mwenye umri ya miaka 24, na kocha wake raia wa Rwanda Gervais Hakizimana walifariki papo hapo walipopata ajali mbaya mwendo wa saa tano za usiku Februari 11, mwaka huu, mtu wa tatu aliyekuwa kwenye gari lao amenusurika.
Kifo chake kimetokea chini ya wiki moja tu baada ya mwanariadha huyo kuidhinisha rekodi yake ya dunia ya mbio za marathon.