Mawakili wa Dkt. Kizza Besigye mwanasiasa maarufu nchini Uganda ambaye ameshtakiwa katika mahakama ya kijeshi nchini Uganda, wamepiga kambi katika Mahakama ya Juu jijini kampala, wakitaka kusikilizwa na Jaji Mkuu Alfonse Owiny-Dollo kuhusu kucheleweshwa kwa leseni ya mazoezi ya aliyekuwa Waziri wa Sheria wa Kenya, Martha Karua nchini Uganda.
Karua na Meya wa Kampala, Erias Lukwago wanaongoza timu ya mawakili wanaomtetea Kiiza Besigye na mwenzake Obeid Lutale.
Karua anahitaji leseni ya muda ya kisheria ili kutoa huduma yake nchini Uganda.
Kesi kuhairishwa
Mahakama ya kjeshi nchini Uganda iliahirisha kesi ya mwanasiasa na mpinzani wa rais Yoweri Museveni, Kiiza Besigye hadi Jumanne, Disemba 10, 2024. Besigye ameshtakiwa na Obeid Lutale kwa makosa yanayohusiana na usalama na kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Hasimu huyo wa kisiasa wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda inadaiwa alichukuliwa kwa nguvu akiwa jijini Nairobi, Kenya na kurudishwa Uganda.
Mawakili wa upande wa utetezi waliomba kuahirishwa kwa kesi ili kutoa muda wa kushughulikia leseni ya muda ya kufanya kazi kwa wakili kiongozi Martha Karua.
Hii ilifuatia mkutano wa faragha kati ya mawakili hao na Besigye ambao ulichukua muda wa dakika thelathini.
Kutokana na hali hiyo, Besigye na Lutale watarejea katika Mahakama ya jeshi tarehe 10 Disemba kwa ajili ya uamuzi na kutajwa kwa kesi yao.
Mawakili 35 wanamtetea Besigye.