Marekani siku ya Alhamisi iliwawekea vikwazo wanajeshi sita wa Kongo na Rwanda wa jeshi au wanamgambo kwa madai ya kushiriki kwao katika kuchochea mzozo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Vita katika eneo hilo limesababisha zaidi ya watu milioni tano na laki tano kukimbia makazi yao nchini DRC.
Katika taarifa, Idara ya Hazina ya Marekani ilisema Brigedia Jenerali Andrew Nyamvumba, Apoilinaire Riaxizimana, Sebastian Uwimbabazi, Ruvugayimikore Protogene kutoka Rwanda pamoja na Bernard Byamungu na Kanali Salomon Tokolonga kutoka Kongo wamekuwa wakivuruga mipaka ya mashariki mwa Kongo kwa miongo kadhaa.
Kundi linaloungwa mkono na Rwanda la March 23 Movement (M23) liliteka sehemu za jimbo la Kivu Kaskazini mwezi Novemba 2021, na kuzidisha mapigano na wanajeshi wa Kongo na wanamgambo wengine ambao wamewakimbia maelfu ya raia.
"Vikwazo vya leo vinaonyesha dhamira ya Marekani ya kuendeleza juhudi za kutatua mzozo huo na kushughulikia hali mbaya ya kibinadamu," Brian Nelson, katibu katika idara ya ugaidi na ujasusi wa kifedha, alisema katika taarifa hiyo.
Unyanyasaji wa kijinsia
"Pande zote katika mzozo zinawajibika kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na, lakini sio tu, kulenga kwa makusudi raia na unyanyasaji wa kijinsia."
Mapigano na majanga ya asili yanayotokea mara kwa mara yamesaidia kuchochea mgogoro wa kibinadamu mashariki mwa Kongo.
Takriban milioni 5.5 wamekimbia makazi yao katika Kivu Kaskazini na majimbo jirani, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.
Jeshi la Kongo halikujibu mara moja ombi la kutoa maoni.
Kundi la M23 halikuweza kupatikana kuzungumzia vikwazo hivyo dhidi ya wanachama wake, wala kundi la Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), kundi jingine la wanamgambo ambalo mwanachama wake aliwekewa vikwazo.