Hamdok

Waziri Mkuu wa zamani wa Sudan Abdalla Hamdok anasema mapigano yanayoendelea nchini humo lazima yaishe mara moja kwa sababu ‘’yana madhara mengi.’’

Bw Hamdok ambaye aliondolewa mamlakani mwaka 2021 na majenerali wawili wanaoongoza vita vya sasa vya kuwania mamlaka, alisema: ''Mungu aepushe mbali ikiwa Sudan itafikia hatua ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kukumba eneo lote...nafikiri itakuwa jinamizi kwa ulimwengu.”

Hamdok alikuwa akizungumza Jumamosi katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, katika Wikiendi ya Utawala Bora wa Ibrahim (IGW), iliyoandaliwa na shirika la Mo Ibrahim, Shirika Lisilo la Kiserikali iliyojitolea kukuza utawala bora barani Afrika.

"Hivi sio vita kati ya jeshi na kundi dogo la waasi, hii ni kama majeshi mawili na yenye mafunzo ya kutosha, yenye silaha," Bw Hamdok alisisitiza.

Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Sudan alitoa wito kwa jeshi la nchi hiyo na wanajeshi hasimu, Rapid Support Forces, kukomesha uhasama. Alisema ili kulinda mpito wa nchi kuelekea utawala wa kiraia '' tunahitaji kuwa na umoja."

Alisisitiza hasa haja ya mashirika ya kiraia na vyama vya kisiasa kufanya kazi pamoja ili kuweka shinikizo kwa jeshi ili kuirejesha nchi katika mkondo wa mpito wa kidemokrasia.

Bw Hamdok, mwanauchumi mashuhuri, alisema kipaumbele cha haraka ni kuwa na usitishaji wa mapigano unaofanya kazi na kisha shinikizo la kudumu la usitishaji wa kudumu.

Alioengeza kuwa hakuna faida kwenye hii ‘‘vita isiyo na maana’’ katika nchi ya tatu kwa ukubwa barani Afrika.

Kulingana na maelezo yake, “kama Wasudan hatutaamini hata kama kundi moja litadai ushindi. Ushindi juu ya maiti na vifo vya watu wako? Ushindi gani huu?”

Abdalla Hamdok alikua mkuu wa serikali ya mpito nchini Sudan kufuatia kupinduliwa kwa mtawala wa muda mrefu wa nchi hiyo Omar al Bashir na jeshi mnamo 2019.

Lakini pia aliondolewa na jeshi mnamo Oktoba 2021, na kurejeshwa mwezi mmoja baadaye kufuatia shinikizo la kimataifa lakini alijiuzulu Januari 2022.

Vita vya kugombea madaraka kati ya majenerali wawili wakuu - Abdul Fatah al Burhan wa jeshi la Sudan na Mohammed Hamdan Dagalo wa Rapid Support Forces vimeua zaidi ya watu 500 na kupelekea mamia kwa maelfu kukimbia nchini - na wengi kuvuka mipaka.

Katika baadhi ya maeneo ndani na nje ya mji mkuu Khartoum, wakazi Jumamosi waliripoti kuwa maduka yalikuwa yakifunguliwa tena na hali ya kawaida kurejea taratibu huku kiwango cha mapigano kikipungua kufuatia kuongezwa kwa mapatano tete.

Lakini katika maeneo mengine, wakazi waliojawa na hofu waliripoti milipuko na milio ya risasi kuwazunguka na wapiganaji wakipora baadhi ya nyumba.

TRT Afrika