Uzalishaji wa chai nchini Rwanda unaongezeka na hili linaonekana katika mapato hasa kutokana na mauzo ya nje ya nchi.
Kulingana na Bodi ya Kitaifa ya Mauzo ya Nje ya Kilimo (NAEB) Uzalishaji wa chai uliongezeka kwa kasi katika miongo kadhaa iliyopita kutoka tani 5,910 za chai iliyoongezwa ubora mwaka 1980 hadi tani 40,003 kufikia Juni 2024.
" Uzalishaji kuongezeka unatokana na majani mabichi yaliyochakatwa ambayo takriban 65% yake hutolewa na wakulima wa chai (wakulima wadogo) huku iliyobaki inatolewa na viwanda vya chai," NAEB ilisema.
Rwanda ilipata dola milioni 114.8 kutokana na mauzo ya chai mwaka 2023/2024, ikiwa ni ongezeko kutoka dola milioni 107.7 katika mwaka wa fedha uliopita, takwimu ya bodi hiyo ilionyesha.
Hii ilitokana na tani 38,460 mwaka 2023/2024, ikiwa imepungua kidogo ikilinganishwa na tani 39,000 katika mwaka wa fedha uliopita.
Bei kwa kilo ya chai ilikuwa dola 2.98, ikiwa ni juu ya kiwango cha dola $2.76 katika mwaka uliopita.
Wanunuzi wa Chai ya Rwanda
Takwimu kutoka NAEB zinaonyesha kuwa chai ya Rwanda ilisafirishwa katika nchi 47 mwaka 2023/2024.
Pakistan inaongoza kama mnunuzi mkubwa ikichukua zaidi ya tani 9,194 kwa takriban dola milioni 27.5.
Uingereza ni ya pili kwa kununua zaidi ya tani 5,669 na kulipa zaidi ya milioni 17.
Nchi zingine ni pamoja na Misri, Ireland, Kazakhstan, Urusi, UAE, Uturuki na India.
Kwa sasa Rwanda inasema kuna zaidi ya hekta 33,000 zilizopandwa chai katika mikoa ya Kaskazini, Magharibi, na Kusini mwa Rwanda zinazomilikiwa na wakulima na viwanda vya chai.
Nchini Rwanda, zaidi ya wakulima 50,000 wa chai wamejumuishwa katika vyama 23 vya ushirika vya chai na makampuni yaliyokubali kununua mavuno ya wakulima. Pamoja na hayo, kuna viwanda 19 vya chai vinavyomilikiwa na watu binafsi.