Majenerali wanaopigana nchini Sudan wamekubali kusitisha vita kwa saa 72 kuanzia Jumapili, wapatanishi wa Marekani na Saudia walisema,
Hii ni Baada ya mapigano kuzidi na mashambulizi mabaya ya anga mjini Khartoum yaliyosababisha kuhama kwa waliojeruhiwa kutoka Darfur kwenye mpaka wa Chad.
Mashambulizi ya anga yameua raia 17, wakiwemo watoto watano, katika mji mkuu wa Khartoum Jumamosi, kundi moja la wananchi lilisema.
Madaktari nchini Chad wameripoti kupokea mamia ya waliojeruhiwa kutoka Darfur wakitafuta matibabu.
Usitishaji mapigano wa hivi punde umeanza Jumapili asubuhi lakini haijulikani iwapo utaendelea.
Makubaliano mengi yamefanywa na kuvunjwa wakati wa vita vya miezi miwili, licha ya Marekani kuwawekea vikwazo majenerali wote wawili baada ya jaribio la awali kuporomoka mwishoni mwa Mei.
Usitishaji vita wa saa 24 kuanzia Juni 10 hadi Juni 11 uliwapa wakazi wa Khartoum afueni kwa muda mfupi kutokana na mashambulizi ya anga na ufyatulianaji wa risasi ambao umeharibu vitongoji vyote vya mji mkuu. Lakini mapigano yalianza tena ndani ya dakika 10 baada ya kumalizika kwa usitishaji huo.
"Ufalme wa Saudi Arabia na Marekani wametangaza makubaliano ya wawakilishi wa vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF) na Vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) kuhusu usitishaji vita kote Sudan kwa muda wa saa 72," taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia ilisema Jumamosi.
Msaada unaohitajika
"Pande hizo mbili zilikubaliana kwamba katika kipindi cha usitishaji vita zingejiepusha na harakati za mashambulizi, matumizi ya ndege za kivita au ndege zisizo na rubani, ufyatuaji wa risasi, upanuzi wa himaya , uongezaji wa vikosi, au kuhujumu juhuzi za kutafuta upatanishi wa vikosi," wapatanishi hao walisema.
"Pia walikubali kuruhusu uhuru wa kutembea na utoaji wa misaada ya kibinadamu kote Sudan."
Jeshi la Sudan, SAF, linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan, tangu Aprili 15 limekuwa likipambana na wanamgambo wa RSF, wakiongozwa na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo, baada ya wawili hao kugombana katika kugombea madaraka.
Takriban watu milioni 25 - zaidi ya nusu ya wakazi wa Sudan - wanahitaji msaada, Umoja wa Mataifa unasema.
Walioshuhudia wanasema mashambulizi ya anga yameongezeka katika mji mkuu katika siku chache zilizopita.
Jumamosi, ndege za kivita zilishambulia wilaya kadhaa za makazi za Khartoum, na kuua "raia 17, wakiwemo watoto watano", kulingana na kamati ya usaidizi ya wananchi.
Waliojeruhiwa watoroka
Katika video iliyochapishwa Ijumaa kwenye ukurasa wa Facebook wa jeshi, naibu mkuu wa jeshi Yasser Atta alionya raia kujiepusha na nyumba za makazi za RSF kwasababu jeshi "litawashambulia wakati wowote".
Siku ya Jumamosi, wizara ya afya ya Sudan ilisema idadi ya waliofariki imefikia 3000.
Kilomita kadhaa magharibi mwa Khartoum, takriban watu 1,100 wameuawa katika mji mkuu wa jimbo la Darfur Magharibi El Geneina pekee, kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Madaktari nchini Chad walisema Jumamosi kulikuwa na mamia ya majeruhi wanaotoroka jimbo la Darfur nchini Sudan.
Waliofariki ni pamoja na Gavana wa Darfur Magharibi Khamis Abdullah Abakar, aliyeuawa baada ya kuwakosoa wanamgambo hao katika mahojiano ya televisheni ya Jumatano.
RSF ilikataa kuwajibika.