Mabaki ya watu 119 wanaoaminika kuwa waathirika wa mauaji ya halaiki ya nchini Rwanda mwaka 1994, yamegunduliwa kusini mwa nchi hiyo, afisa mmoja wa nchi hiyo ameliambia Shirika la Habari la Associated Press.
Makaburi hayo yaligunduliwa siku ya Alhamisi, karibu miongo mitatu baada ya wimbi la ghasia za kikabila na kusababisha vifo vya Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani, lililotokea kati ya Aprili 7 na Julai 15, 1994.
''Mabaki ya waathiriwa zaidi yanaendelea kupatikana kwa sababu wahusika wa mauaji ya halaiki walijaribu kuficha taarifa zinazoweza kuwa za hatia,'' alisema Naphtal Ahishakiye, Katibu mtendaji wa shirika la waathirika wa mauaji ya kimbari Ibuka.
Mnamo Oktoba mwaka jana , mabaki ya miili sita ya waathirika wa mauaji hayo ilipatikana chini ya nyumba iliyokuwa inaendelea na ujenzi katika wilaya ya Huye.
Miili zaidi ilipatikana kufuatia uchunguzi zaidi.
Louise Uwimana, manusura wa mauaji ya halaiki na mkazi wa wilaya ya Huye, alisema alisikitishwa baada ya kugundua kuwa majirani zake walimficha kuhusu taarifa za uwepo wa makaburi hayo wakati Serikali inahimiza maridhiano.
Aprili mwaka huu, Rwanda itaadhimisha kumbukumbu ya miaka 30 ya mauaji ya halaiki, ambapo mashada ya maua yatawekwa kwenye makaburi ya waathirika wa machafuko hayo.