Majirani wa Gabon wanatarajiwa kufanya mkutano usio wa kawaida baada ya wanajeshi walioasi katika taifa hilo la Afrika ya Kati kusema wamechukua mamlaka na kumweka rais Ali Bongo Ondimba katika kizuizi cha nyumbani.
Bado haijafahamika ni lini na wapi mkutano wa jumuiya ya kanda ya Afrika ya Kati (ECCAS) utafanyika.
Lakini jumuiya hii imetaka kikundi cha wanajeshi Gabon kurejesha kwa haraka nchi hiyo kwa utaratibu wa kikatiba.
Umoja huo katika taarifa pia umelaani matumizi ya nguvu kama njia ya kutatua migogoro ya kisiasa na kupata mamlaka.
Wanajeshi wa Gabon wamemtaja Jenerali Brice Oligui Nguema kuwa kiongozi mpya wa nchi hiyo.
Uchaguzi usio wa haki
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema mapinduzi ya kijeshi nchini Gabon hayawezi kulinganishwa na mzozo wa Niger, akidai kuwa wanajeshi waliingilia kati baada ya rais aliyepinduliwa Ali Bongo kushinda uchaguzi usio wa haki.
"Kwa kawaida, mapinduzi ya kijeshi sio suluhu, lakini hatupaswi kusahau kwamba nchini Gabon kumekuwa na uchaguzi uliojaa dosari," alisema Alhamisi, akisema kura iliyoibiwa inaweza kuwa "mapinduzi ya taasisi" ya kiraia.
Borrell alikuwa akizungumza kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya ambapo walipaswa kujadili jinsi ya kusaidia kundi la kanda ya Afrika Magharibi la ECOWAS kushughulikia unyakuzi wa kijeshi wa Julai 26 nchini Niger.
Umoja wa Afrika umelaani mapinduzi ya hivi punde na mamlaka kuu ya kikanda Nigeria imeelezea wasiwasi wake juu ya " utawala usiofuata katiba " kufuatia matukio kama hayo huko Niger na Mali.