Shirika la kimataifa la uhamiaji - International Migration Organisation (IOM) inasema nchini Sudan, takriban watu milioni 4.8 wamekimbia makazi yao ndani na nje ya nchi kutokana na mzozo uliozuka tarehe 15 Aprili.
Vita kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha Rapid Support Forces inaendelea,
Zaidi ya watu milioni 3.8 wamehama makwao ndani ya nchi kufikia tarehe 29 Agosti.
"Aidha, takriban watu 963,000 wamevuka mpaka na kuingia nchi jirani kufikia tarehe 2 Agosti, ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini, " kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
Kati ya hawa takriban watoto milioni 2 wamelazimika kuyahama makazi yao tangu mzozo nchini Sudan ulipozuka zaidi ya miezi minne iliyopita, na wastani wa zaidi ya watoto 700 wanayahama makazi yao kila saa.
Takriban watoto milioni 14 wanahitaji msaada wa kibinadamu kwa dharura, huku wengi wakikabiliwa na vitisho vingi kama vya afya.
Mbali na maeneo yenye mizozo kama vile Darfur na Khartoum, mapigano hayo sasa yameenea katika maeneo mengine yenye wakazi, ikiwa ni pamoja na Kusini na Magharibi mwa Kordofan, yakizuia utoaji na upatikanaji wa huduma za kuokoa maisha kwa wale wanaohitaji dharura.