Wakazi hao walionesha hisia zao wa wazi wakati wa maandamano yao ya amani ambayo kwa kiasi fulani, yalitatiza shughuli za utalii kati ya Ngorongoro na Serengeti, hivi karibuni./Picha: TRT Afrika  

Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Arusha imezuia tamko la Serikali namba 673 la Agosti 2, 2024 la kufuta kata, vijiji na vitongoji vya wilaya ya Ngorongoro hadi mahakama hiyo itakavyoelekeza vinginevyo

Jaji wa Mahakama hiyo Ayoub Mwenda ametoa maamuzi hayo siku ya Agosti 22, 2024 kufuatia maombi yaliyowasilishwa na mmoja ya wananchi wa Ngorongoro, Isaya Ole Posi.

Hivi karibuni, katika tangazo la Serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) wa Tanzania, Mohamed Mchengerwa alitangaza kuvifuta vijiji vyote ndani ya tarafa ya Ngorongoro, iliyoko Arusha, Tanzania.

Katika taarifa yake, Waziri huyo alitangaza hatua ya kuvifuta vijiji vyote vilivyomo ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, kama hatua ya kuendelea na mchakato wa kuwahamisha wakazi wa eneo hilo kuelekea kijiji cha Msomera, kilichopo Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Tanzania.

Tarafa ya Ngorongoro ambayo inakaliwa na jamii ya wafugaji wa jamii ya Kimaasai ina jumla ya vijiji 25, kata 11 na vitongoji 96.

TRT Afrika