Oktoba 2023 Wizara ya Kilimo nchini Kenya ilipiga marufuku uuzaji nje wa parachichi na karanga za makadamia.
Marufuku ya mauzo ya makadamia na mavuno yangeanza kutoka Novemba 2, 2024 hadi Machi 1, 2025. Waziri alidai uvunaji, usindikaji na usafirishaji wa karanga ambazo hazijakomaa huathiri mapato ya mazao kutoka Kenya katika soko la kimataifa.
Ili kuhakikisha wakulima hawakosi haki yao Andrew Karanja, ambae ni Waziri wa Kilimo nchini Kenya alisema kuwa serikali itaanzisha bei ya chini ya dhamana kwa mazao yanayouzwa katika soko la ndani.
Hata hivyo Mahakama nchini humo imefuta marufuku hiyo.
Jaji wa Mahakama ya Juu Lawrence Mugambi mnamo Ijumaa alisitisha agizo lililotolewa na Waziri wa Kilimo Andrew Karanja, kufuatia kesi iliyowasilishwa na mtetezi wa wakulima wa makadamia Erick Mwirigu Mbaabu na Kampuni ya Edenswin Traders Limited Novemba 13, 2024.
"Mlalamikiwa amezuiwa kuingilia haki za umiliki za wakulima wa makadamia, wafanyabiashara na wauzaji nje wa karanga zilizosindikwa kwenye ganda la makadamia," aliamuru Jaji.
Walalamishi hao walilaumu kuwa karanga katika kaunti za Meru, Embu, Nyeri na Kirinyaga tayari zimekomaa kinyume na madai ya Waziri Karanja, na hivyo hiyo haiwezi kusubiri hadi Machi mwaka ujao kuvunwa.
Mwirigi alidai kuwa Waziri hana mamlaka ya kusimamisha uvunaji wa bidhaa hiyo kama ilivyo katika agizo lake la Oktoba 22, 2024.
"Agizo la mawaziri ni la ukandamizaji, halikubaliki, haramu na lina mwelekeo wa kupendelea wasindikaji na litawanyima haki wakulima wa karanga kwa kuleta uhaba wa soko bandia, bei ya chini, kuunda ukiritimba, na itawanufaisha wasindikaji pekee," alisema.
Alidai pia kuwa agizo hilo limetolewa bila kushirikisha wananchi wala kushauriana na wakulima kote nchini.
Kenya husafirisha sehemu kubwa ya karanga na matunda katika Mashariki ya Kati na Ulaya pamoja na Uchina. Parachichi ndio tunda kuu ambalo nchi hiyo inauza nje.
Karanga za makadamia, ambazo mara nyingi hujulikana kama ‘mfalme wa karanga,’ zimeshuhudia ongezeko la mahitaji katika soko la kimataifa kutokana na ladha yake na manufaa ya kiafya.