Mahakama nchini Kenya imetenga Novemba kama mwezi wa Kitaifa wa haki kwa watoto nchini. Katika mwezi huu jaji mkuu Martha Koome amesema utakuwa mwezi wa kuzipa kipaumbele kesi zote zinazohusisha watoto.
Koome alivumbua mwezi huu katika hafla iliyofanyika katika kaunti ya Kiambu.
" Leo, tunapojitolea kwa mwezi huu wa kuzingatia watoto zaidi, tunajitolea pia kuchukua hatua ambazo zitafanya haki ya mtoto aweze kurejeshwa zaidi katika jamii badala ya kumuadhibu," Koome aliwaambia wanasheria wenzake.
Wanasheria wamesema uchunguzi wa awali na ucheshi ni mazoea yanayoheshimu hali mahususi ya kila mtoto, na kuwapa nafasi ya kushughulikia sababu za msingi za mgongano wao na sheria.
Amesema mafanikio ya mageuzi ya tabia wa mtoto yanatokana na ushirikiano.
"Kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), Idara ya Huduma za Watoto (DCS), na Idara ya Marejeleo, naomba ushirikiano wa karibu na wataalamu wa afya na saikolojia. Ushirikiano huu utaimarisha uwezo wetu wa pamoja wa kusaidia, kurekebisha, na kuwajumuisha upya watoto kwa ufanisi," Koome ameongezea.
Ameshauri kuwa katika mfumo wa utoaji haki, wanaposubiri kukamilika kwa Sheria ya Watoto wanaokinzana na Sheria, ni muhimu kushirikiana kutekeleza uchunguzi wa awali, mikutano ya vikundi vya familia na kuwarudisha kwa jamii watoto wanaokinzana na sheria.
"Tunaposhughulikia ulinzi na utu wa watoto wanaokinzana na sheria, dhamiri zetu haziwezi kupuuza vivuli vilivyowekwa katika jamii yetu na janga linaloongezeka la mauaji ya wanawake. Wanawake na wasichana katika jamii zetu—wale ambao ni binti zetu, dada zetu, mama zetu na marafiki—wanavumilia ukatili usioelezeka," Jaji mkuu Koome alisema.