Wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma nchini Kenya wanafanya mgomo wakitaka serikali itimize ahadi ya kuongeza mishahara / Picha: Reuters

Masomo katika vyuo vikuu vyote vya umma nchini Kenya yamesalia kulemazwa huku wahadhiri wakiapa kutorudi kazini hadi matakwa yao yatakapotimizwa.

Mgomo huo ulioanza Jumanne, Oktoba 29, 2024, na umetatiza masomo na mitihani.

Wahadhiri chini ya Muungano wa Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (UASU) walianza mgomo Jumanne wakiitaka serikali kuzingatia matakwa yake kama ilivyoainishwa katika Makubaliano ya Pamoja ya Majadiliano ya 2012-2025 (CBA).

"Hatutafundisha, kuashiria, au kusimamia mitihani hadi serikali itakapoheshimu makubaliano," alitangaza Dkt. Constatine Wesonga, Katibu Mkuu wa UASU.

UASU inasema mgomo wa wahadhiri utamalizika ikiwa watapokea nyongeza ya mishahara iliyokubaliwa ya kati ya 7-10%.

"Tunafahamu serikali imekuwa ikipanga bajeti ya nyongeza ya kila mwaka ya asilimia nne, lakini haijakuwa ikiwalipa wanachama wetu."

UASU inadai kuwa kuna tofauti kubwa kati ya wahadhiri wa vyuo vikuu na wafanyakazi wengine wa utumishi wa umma, na walimu, ambao wamepata nyongeza za kila mwaka moja kwa moja hadi asilimia 8.

"Changamoto kati yetu na UASU kuhusu mfumo ya kurejea kazini kwa wahadhiri ni kwamba tulikubaliana juu ya nyongeza ya 7% na 10% . Lakini takwimu ambayo Serikali inayo dhidi ya takwimu ya UASU inatofautiana kwa takriban zaidi ya 38,759,689 (Kshs 5 bilioni) ," Waziri wa Elimu Julius Migosi ameliambia Bunge la Seneti.

Mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Kazi nchini Kenya imetangaza mgomo unaoendelea wa wahadhiri kusitishwa na kuwaagiza maafisa wake kurudi kwenye meza ya mazungumzo.

UASU na wahusika wote wamepewa siku 14 kuwasilisha jibu kuhusu suala hilo.

Kesi hiyo itatajwa Novemba 28, 2024.

TRT Afrika