Baraza la Mawaziri nchini Kenya limeidhinisha mpango wa kuimarisha mazingira mazuri kwa wasafiri katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kuhakikisha kuna usalama wa kutosha.
Mabadiliko muhimu ni pamoja na kuwaondoa raia wote wa bara la Afrika kutoka kwa Mahitaji ya Uidhinishaji wa Kielektroniki wa Usafiri (ETA) na kurahisisha usafiri ndani ya bara hilo.
Raia wa Kenya watapunguziwa mzigo wa kodi, na sasa kima cha bidhaa wanazoingiza nchini kinachotozwa kimeongezeka kutoka dola 387( KSh50,000 hadi dola 1,936 (KSh250,000).
Ukaguzi wa usalama katika uwanja wa JKIA utaimarishwa kupitia vigezo vya kuzingatia hatari ya mtu, na kuonesha uhakika wa hali hiyo. Mifuko pekee iliyotiwa alama itakaguliwa kwa mikono katika ukaguzi maalum na hapo kupunguza ucheleweshaji na kuimarisha ufanisi.
Ili kuharakisha zaidi usafiri, idadi ya vizimba na maafisa wa uhamiaji vitaongezwa.
Milango ya kutumia teknolojia itaainishwa yaani E-Gates ili kupunguza foleni ndefu na kuongeza kasi ya watu kuingia nchini.
Hatua za uwajibikaji zitatumika pia kama kuimarishwa kwa teknolojia mpya ya ufuatiliaji wa wafanyakazi wa uwanja wa ndege, na sare zao lazima ziwe na majina yanayoonekana, vitambulisho vitahitajika kwa wafanyakazi wote .