Waandamanaji katika jiji la Nairobi wanaopinga utekwaji nyara wa watu, washikiliwa na polisi / Picha: AFP

Polisi katika mji mkuu wa Kenya Nairobi wamerusha mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakiandamana siku ya Jumatatu kupinga kile wanachosema kuwa ni wimbi la utekaji nyara usioelezeka wa wakosoaji wa serikali.

"Kumekuwepo na matukio kumi na tatu (13) zaidi ya utekaji nyara au kupotea kwa watu katika kipindi cha miezi mitatu na kufanya jumla ya kesi 82 kuanzia Juni 2024," Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya imesema katika taarifa.

Kesi saba za utekaji nyara za hivi karibuni ziripotiwa katika mwezi wa Disemba 2024 ambapo sita kati yao wakiwa bado hawajulikani walipo, hivyo kufikisha idadi ya watu 29 ambao hawajapatikana tangu Juni 2024.

Mashirika ya usalama nchini Kenya yamelaumiwa. Hata hivyo, huduma ya taifa ya polisi na kitengo cha makosa ya jinai zimekana tuhuma hiyo.

Mamlaka za Kenya zimesema kuwa serikali haikubaliani na wala haishiriki katika mauaji ya kiholela au utekaji nyara.

Baadhi ya makundi ya vijana waliandamana katikati mwa jiji la Nairobi huku wengine wakipanga kukaa na kuimba kauli mbiu dhidi ya serikali, huku baadhi wakiwa na mabango ya kukashifu kuzuiliwa kuandamana kinyume cha sheria.

Waandamanaji katika mji wa Nairobi wapinga watu kutekwa nyara/ picha: Reuters 

Msemaji wa Polisi wa Taifa hakujibu mara moja ombi la kutoa maoni yake juu ya maandamano ya Jumatatu.

Matukio hayo ya utekaji nyara yalifuatia maandamano ya kuipinga serikali yaliyoanza Juni mwaka huu.

Hapo awali yalilenga kubatilisha mapendekezo ya nyongeza ya ushuru, maandamano hayo hatimaye yalibadilika na kuwa vuguvugu lililokumba migawanyiko ya kitamaduni ya Kenya, na kuwa tishio kubwa kwa serikali ya Rais aliye madarakani William Ruto.

Jaji Mkuu wa zamani atia neno

"Mwaka huu haujakuwa rahisi kwa familia nyingi. Mauaji, ulemavu na utekaji nyara wa vijana wa Kenya umeweka mtihani mkubwa katika taasisi zetu," Jaji mkuu wa zamani David Maraga amesema katika ujumbe wake wa mwaka mpya kwa Wakenya.

Jaji mkuu wa za zamani Kenya Peter Maraga./ Picha: / AFP / SIMON MAINA

"Nalaani mauaji, utesaji na utekaji nyara na kutoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa vijana ambao bado wanashikiliwa kinyume cha sheria," ameongezea.

Kiongozi huyo wa zamani katika sekta ya mahakama anakumbukwa kwa kubatilisha ushindi wa uchaguzi wa 2017 ambapo rais Uhuru Kenyatta na makamu wake walikuwa wametangazwa washindi.

"Natoa wito kwetu sote kutafakari juu ya ahadi tuliyojiwekea katika Katiba yetu ya 2010. Wacha tuamue kuwa mnamo 2025 maadili haya yatakuwa sehemu yetu isiyoweza kutenganishwa," Maraga amesema.

"Lazima tusimame kidete kutetea katiba, utawala wa sheria na haki."

TRT Afrika