Rais Ali Bongo ameongoza Gabon tangu mwaka wa 2009  / Picha: AFP

Marais wa Angola na Kongo Brazzaville wamelaani mapinduzi ya kijeshi nchini Gabon, ambapo jeshi lilimwondoa madarakani Rais Ali Bongo.

Kundi la maafisa wakuu wa jeshi la Gabon walijitokeza kwenye televisheni ya taifa siku ya Jumatano na kutangaza kuwa wametwaa mamlaka na kumweka Bongo katika kizuizi cha nyumbani.

Rais wa Angola, Joao Lourenco na mwenzake wa Jamhuri ya Kongo Denis Sassou Nguesso, walijadili mzozo wa kisiasa nchini Gabon katika mkutano wa Alhamisi katika mji wa Oyo nchini Kongo, zaidi ya kilomita 400 (maili 248.5) kutoka mji mkuu Brazzaville.

Taarifa ya rais wa Kongo ilisema wakuu wa nchi walitaka "kuheshimiwa kwa uadilifu wa kimwili wa Rais Bongo, wa familia yake na wapendwa wake, pamoja na maafisa wakuu wa taasisi."

"Wakuu wa nchi wanawataka wahusika wote kutumia mbinu za kisiasa ili kulinda amani, umoja na utulivu wa watu wa Gabon."

Majeshi wamemtangaza jenerali Brice Oligui Nguema kama rais wa mpito wa nchi hiyo/ Picha AFP

Lourenco na Sassou Nguesso pia walitoa wito wa kuitishwa kwa mkutano wa haraka wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (ECCAS) ili kulipatia shirika hilo uongozi ili kuepusha ombwe la kisheria ambalo linaweza kukwamisha shughuli zao kufuatia mapinduzi ya Gabon.

Mnamo Februari, Bongo alichukua uenyekiti wa zamu wa mwaka mmoja wa jumuiya hiyo.

Umoja wa Afrika yasimamisha uanachama wa Gabon

Umoja wa Afrika , Alhamisi, ilisimamisha uanachama wa Gabon kufuatia mapinduzi ya serikali nchini humo.

"Umoja wa Afrika, ambao una nchi wanachama 55, umeamua kusitisha ushiriki wa Gabon katika shughuli zote za AU, vyombo na taasisi zote za AU hadi kurejeshwa kwa utaratibu wa kikatiba nchini humo," taarifa kutoka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ulisema.

"Umoja wa Afrika inalaani vikali unyakuzi wa kijeshi katika Jamhuri ya Gabon, ambao ulimwondoa madarakani rais Ali Bongo," taarifa hiyo iliongeza.

Gabon ni nchi ya hivi karibuni Afrika kutwaa mamlaka ya kijeshi baada ya wanajeshi wa Niger kunyakua mamlaka mwishoni mwa mwezi uliopita.

TRT Afrika