Paul Mackenzie, mhubiri tata wa ibada ya njaa nchini Kenya ambayo ilisababisha vifo vya zaidi ya watu 400, siku ya Ijumaa alipatikana na hatia ya kuendesha studio na kusambaza filamu bila leseni.
Hakimu mkazi mkuu katika mji wa Malindi, Olga Onalo, alimkuta Mackenzie na hatia ya kuonyesha filamu kupitia televisheni yake ya 'Times' bila idhini ya Bodi ya Kuainisha Filamu nchini Kenya.
Mhubiri huyo amekuwa akizuiliwa na polisi kwa zaidi ya miezi sita sasa tangu alipokamatwa mwezi wa Aprili, kufuatia kupatikana kwa mamia ya miili katika makaburi ya halaiki katika eneo lenye msitu katika eneo lake la ekari 800 katika kaunti ya pwani ya Kilifi.
Waendesha mashtaka wanasema Mackenzie aliamuru waumini wake kufa kwa njaa ili kukutana na Yesu.
Bado mashtaka
Hata hivyo, hajafunguliwa mashtaka rasmi kuhusu vifo hivyo, licha ya kufikishwa mahakamani mara kadhaa tangu akamatwe.
Siku ya Ijumaa alifutiwa mashtaka ya ziada ya kushawishi watoto kutohudhuria shule na kutumia mahubiri makali kuwachochea Wakristo dhidi ya Wahindu, Wabudha na Waislamu.
Atahukumiwa kwa makosa yanayohusiana na filamu mnamo Desemba 1 na anaweza kufungwa jela miaka mitano.
Siku ya Alhamisi, waendesha mashtaka waliomba Mackenzie azuiliwe kwa miezi sita zaidi ili kuruhusu polisi kukamilisha uchunguzi wao ambao ni pamoja na kutafuta makumi ya watu ambao bado hawajapatikana.
Tangu kukamatwa kwake, kumekuwa na wito kwa serikali kudhibiti makanisa nchini Kenya.