Mahakama nchini Kenya imemshtaki kiongozi wa kundi la waumini wa njaa na wengine wanaoshukiwa kuhusika na mauaji kutokana na vifo vya takriban watu 200 katika msitu wa Shakahola , pwani mwa Kenya.
Aliyejiita kasisi Paul Nthenge Mackenzie, ambaye tayari amefunguliwa mashtaka ya ugaidi, kuua bila kukusudia na vile vile kutesa watoto na ukatili, anadaiwa kuchochea mamia ya wafuasi wake kufa kwa njaa kwa madai kuwa "watakutana na Yesu."
Siku ya Jumanne, Mackenzie na washukiwa wengine 29 walikana mashtaka 191 ya mauaji, kulingana na hati za mahakama.
Mshukiwa wa 31 alichukuliwa kuwa hana uwezo wa akili wa kujibu mashtaka na kuamriwa arudi katika Mahakama Kuu ya Malindi baada ya mwezi mmoja.
Kiongozi huyo wa ibada amekana mashtaka yote dhidi yake.
Mackenzie alikamatwa mwezi Aprili mwaka jana baada ya miili ya wafuasi wake kupatikana katika msitu wa Shakahola, hali iliyozua taharuki duniani kote.
Uchunguzi wa maiti ulionyesha kuwa wengi wa wahasiriwa 429 walikufa kwa njaa. Lakini wengine, wakiwemo watoto, walionekana kunyongwa, kupigwa au kuzidiwa.
Kesi hiyo, iliyopewa jina la "mauaji ya msitu wa Shakahola", ilisababisha serikali kuashiria hitaji la udhibiti mkali wa madhehebu tofauti.
Kudhibiti makanisa
Mahakama zimeelezea kuwa kanisa la Good News International Ministries iliyoanzishwa na Mackenzie kama "kundi la uhalifu lililopangwa, ambalo lilijihusisha na vitendo vya uhalifu vilivyopangwa", na kusababisha vifo vya mamia ya wafuasi.
Maswali yameibuka kuhusu jinsi Mackenzie aliweza kukwepa utekelezaji wa sheria licha ya historia ya itikadi kali na kesi za awali za kisheria.
Tume ya uchunguzi ya Seneti iliripoti mnamo Oktoba kwamba baba huyo wa watoto saba alikabiliwa na mashtaka mwaka wa 2017 kwa kuhubiri kupita kiasi.
Aliondolewa mashtaka ya itikadi kali mwaka 2017 kwa kutoa mafundisho ya shule kinyume cha sheria baada ya kukataa mfumo rasmi wa elimu ambao alidai hauendani na Biblia.
Mnamo mwaka wa 2019, alishtakiwa pia kwa kuhusishwa na kifo cha watoto wawili wanaoaminika kufa kwa njaa, kukosa hewa na kisha kuzikwa kwenye kaburi la kina huko Shakahola.
Aliachiliwa kwa dhamana akisubiri kesi yake. Kuna zaidi ya makanisa 4,000 yaliyosajiliwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki yenye watu milioni 53, kulingana na takwimu za serikali.
Juhudi za hapo awali za kudhibiti taasisi za kidini nchini Kenya zimepingwa vikali huku juhudi za kudhoofisha uhakikisho wa kikatiba wa mgawanyiko wa kanisa na serikali.