Wanamgambo waliwauwa takriban wanakijiji 12 katika msururu wa mashambulio mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, afisa wa eneo hilo na kiongozi wa mashirika ya kiraia amesema huku rais wa nchi hiyo akifutilia mbali mazungumzo na nchi jirani ya Rwanda kuhusu mzozo unaohusiana na eneo hilo.
Mauaji hayo katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini Congo yalifanyika siku ya Jumanne na yanadaiwa kufanywa na kundi la Allied Democratic Forces, wanamgambo wenye silaha wanaoaminika kuwa na uhusiano na kundi la Daesh.
Wanamgambo hao walishambulia vijiji vitatu katika eneo la Beni, kulingana na Kinos Katuho, rais wa Shirika la Kiraia la Mamove.
Mashariki mwa Congo imekuwa ikikabiliwa na ghasia za kutumia silaha kwa miongo kadhaa huku zaidi ya makundi 120 yakipigania mamlaka, ardhi na rasilimali muhimu za madini, huku wengine wakijaribu kutetea jamii zao.
Kuanzishwa upya kwa M23
Makundi yenye silaha kwa muda mrefu yamekuwa yakiendesha kampeni za ghasia katika eneo hilo lenye utajiri wa madini na yamekuwa yakishutumiwa kwa mauaji ya halaiki.
Mzozo huo uliongezeka mwishoni mwa 2021 wakati kundi jengine la waasi, ambalo linaitwa M23, lilipoibuka tena na kuanzisha mashambulizi ili kuteka eneo.
Kundi hilo linadaiwa kuungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda, ingawa nchi hiyo inakanusha uhusiano huo.
"Watu wawili waliuawa katika kijiji cha Mangazi-Kasongo, watano katika eneo la Matadi-Beu na wengine watano Mamove," alisema Katuho.
Miongoni mwa waliouawa na washambuliaji - ambao pia walipora mali - alikuwa chifu wa kijiji cha Matadi-Beu, kulingana na chifu wa Mamove Charles Endukadi.
'Hakuna mazungumzo'
Wakati huo huo, Rais wa Congo Félix Tshisekedi Jumanne alirudia madai yake kwamba waasi wa M23 wanaungwa mkono na Rwanda, na kusema hatashiriki mazungumzo na kiongozi wa Rwanda, Paul Kagame, kuhusu suala hilo.
Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu pia yamesema wanamgambo hao wanapata uungwaji mkono kutoka Rwanda. Hata hivyo, Rwanda, mara kadhaa imekanusha tuhuma hizo.
"Hakuna mazungumzo yatakayofanyika na mchokozi mradi anachukua sehemu ya eneo letu," Tshisekedi alisema, akimaanisha Rwanda.
Alizungumza wakati wa mkutano na wanadiplomasia katika mji mkuu wa Congo wa Kinshasa.