Afrika Kusini na Israeli zitakabiliana katika Mahakama Kuu ya Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi ambapo majaji watasikiliza kesi ya Afrika Kusini inayoishutumu Israeli kwa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza na kuomba kusitishwa kwa dharura kwa kampeni ya kijeshi ya Israel.
Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mjini Hague, ambayo pia inajulikana kama Mahakama ya Dunia, itakuwa na siku mbili za kusikilizwa wiki hii katika kesi iliyowasilishwa mwishoni mwa Disemba ikiishutumu Israel kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari ya 1948.
Israeli imeitaja kesi nzima kuwa ya kipuuzi na kuishutumu Pretoria kwa kucheza kama "wakili wa shetani" wa Hamas, kundi la upinzani la Palestina ambalo linaendesha vita dhidi yake huko Gaza.
Afrika Kusini na Israeli ni wanachama wa Mkataba wa Mauaji ya Kimbari, ambao unawalazimu wanachama kutofanya mauaji ya halaiki na pia kuyazuia na kuyaadhibu.
Mkataba huo unafafanua mauaji ya halaiki kama, "vitendo vilivyofanywa kwa nia ya kuharibu, kwa ujumla au kwa sehemu, kikundi cha kitaifa, kikabila, rangi au kidini."
Sitisha hatua za kijeshi
Afrika Kusini imeiomba mahakama kuamuru msururu wa hatua za dharura ikiwa ni pamoja na kusitishwa kwa hatua za kijeshi huko Gaza wakati mahakama hiyo ikisikiliza kesi hiyo kwa kuzingatia haki, ambayo inaweza kuchukua miaka.
Vikosi vya Israel vilianzisha mashambulizi yao baada ya wapiganaji kutoka Gaza inayotawaliwa na Hamas kutekeleza shambulio la Oktoba 7 kuvuka mpaka ambapo Israeli inasema watu 1,200 waliuawa na 240 kutekwa nyara.
Tangu wakati huo, mashambulizi hayo yamepelekea sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza wenye wakazi wengi kuharibiwa, na takriban watu wake wote milioni 2.3 kukosa makazi, na kusababisha janga la kibinadamu.
Afrika Kusini baada ya ubaguzi wa rangi wa muda mrefu imekuwa ikitetea dhamira ya Palestina, uhusiano ulioanzishwa wakati wa mapambano ya chama cha African National Congress dhidi ya utawala wa weupe walio wachache ulienziwa na chama cha Yasser Arafat cha Ukombozi wa Palestine.
Sitisha mahusiano
Mwezi Novemba, Chama Tawala cha ANC kiliunga mkono hoja katika bunge la nchi hiyo ya kusitisha uhusiano wa kidiplomasia na Israeli hadi ikubali kusitishwa kwa mapigano huko Gaza.
Katika mjalada wake mahakamani, Afrika Kusini inataja kushindwa kwa Israeli kutoa chakula, maji, dawa na misaada mingine muhimu ya kibinadamu katika eneo la Palestina.
Pia inaashiria kampeni endelevu ya ulipuaji wa mabomu ambayo imeua zaidi ya watu 23,000 kulingana na mamlaka ya afya ya Gaza.
Msemaji wa Serikali ya Israel Eylon Levy amesema kabla ya kusikilizwa kwa kesi hiyo kwamba Israel "inaendelea kujitolea na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za kimataifa," na kusisitiza kwamba hatua zote za kijeshi zinaelekezwa dhidi ya Hamas. Uamuzi wa hatua za dharura unatarajiwa baadaye mwezi huu.
Mahakama haitatoa uamuzi wakati huo kuhusu madai ya mauaji ya halaiki, kwani kuna uwezekano wa miaka kadhaa kupita kabla ya hukumu kutolewaa. Maamuzi ya ICJ ni ya mwisho na hayana rufaa lakini mahakama haina njia ya kuyatekeleza.