Wizara ya Afya nchini Kenya imetoa taarifa kuhushu ripoti kuwa kuwepo kwa ongezeko la hivi majuzi la maambukizi ya homa ya mafua, haswa ikizingatia kuongezeka kwa visa vya mafua na kuendelea kufuatilia visa vya Uviko 19.
Wizara ya Afya inasema mafua yameongezeka kati ya Februari na Machi.
Dk. Patrick Amoth, Mkurugenzi Msimamizi Mkuu wa Afya, amewataka wananchi kuwa makini na kufuata ushauri wa Wizara ili kuzuia maambukizi hayo.
Amesema licha ya ripoti za maambukizi ya mfumo wa upumuaji, hakujawa na ongezeko kubwa la kesi za Uviko-19.
Wizara ya Afya imesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za tahadhari, ikiwa ni pamoja na kuepuka kuwasiliana kwa karibu na wagonjwa, kufanya mazoezi ya kupumua na usafi wa mikono, kuvaa barakoa katika maeneo ya umma, na kuzingatia chanjo ya mafua.
Wizara imeendelea kusema, kuwa kuna umuhimu wa uangalifu maalumu hasa kwa vikundi vilivyo hatarini, kama vile watoto, wazee, wanawake wajawazito na wale walio katika hali mbaya ya kiafya.