Awamu ya tatu ya ufukuaji wa miili imeanza katika msitu wa Shakahola , katika kaunti ya Kilifi, mashariki mwa Kenya.
Miili tisa tayari imetolewa katika zoezi hilo lililoanza tena Jumanne.
Serikali inaendelea kuwasaka watu ambao huenda walizikwa katika msitu huo baada ya kufa kwa kujinyima chakula wakiamini ibada ya njaa.
"Tumegundua kuwa Mackenzie anaweza kuendeleza uhalifu wake zaidi ya ekari 800," waziri wa mambo ya ndani, Kithure kindiki alimesema," tunazingatia kuendeleza uchunguzi kwa zaidi ya ekari 37,000 katika eneo la shamba la Chakama. Katika kila ekari 100 kutakuwa na kambi ya usalama, kuwezesha uchunguzi wa kina na wa kisayansi."
Msitu wa Shakahola ni sehemu ya shamba kubwa la Chakama.
Hadi sasa watu 251 wamekufa kutokana na ibada hiyo ya njaa wengi wao walikutwa wamezikwa sehemu tofauti katika msitu wa Shakahola ambao una ukubwa wa ekari 800.
Watu 613 waliripotiwa kupotea wakati uchunguzi ulianza mwezi Aprili.
Serikali ilikuwa imesitisha ufukuaji wa miili kwa muda mwezi Aprili huku ikifanya uchunguzi wa kiafya ya miili iliyokuwa tayari imefukuliwa.
Sampuli za DNA zimekusanywa kutoka kwenye miili 93 ili kubaini miili ambayo haija tambuliwa
Takriban watu 95 waliokolewa wakiwa hai.
Watu 45 wamekamatwa akiwemo kiongozi wa ibada hiyo, Paul Mackenzie.