Wizara ya Afya ya Kenya imesema imepokea zaidi ya dozi milioni nane za chanjo ya watoto huku chanjo ikiripotiwa kuendelea kupungua nchini.
Wizara hiyo inasema imetenga zaidi ya dola milioni 9.5, kununua chanjo za watoto kwa haraka. Hii inafuatia upungufu wa chanjo nchini, jambo ambalo limepaziwa sauti na vyombo vya habari nchini humo.
"Chanjo zilizopokewa kwa sasa zinachakatwa kwa usambazaji wa haraka katika vituo vya chanjo maeneo tisa kote nchini. Ili kuharakisha mchakato huu, wizara ya afya imetumia malori ya ziada ya friji ili kuhakikisha chanjo hizi za kuokoa maisha zinarejeshwa vituoni na jumuiya zetu za afya ifikapo wiki ya pili ya Juni 2024," ameeelezea Katibu Mkuu wa Huduma za Matibabu katika Wizara ya Afya, Harry Kimtai.
“Kufikia leo tumepokea dozi 1,209,500 za surua , dozi 3,032,000 za polio, dozi 1,000,000 za Diphtheria na pepopunda , na dozi 3,129,000 dhidi ya BCG,” Kimtai ameongezea.
Uhaba mkubwa wa chanjo, ulioripotiwa mwanzoni mwa Mei, ulileta hatari ya watoto kuambukizwa magonjwa hatari lakini yanayoweza kuzuilika kama vile surua, polio, pepopunda na kifua kikuu.
Licha ya ripoti za awali kuhusisha upungufu huo na ufadhili uliopunguzwa wa wafadhili kutoka kwa mashirika kama Gavi na UNICEF, ununuzi wa hivi punde wa chanjo umepatikana kupitia Muungano wa Chanjo ya Gavi.
Chanzo za uhaba wa chanjo?
Wizara imesema itashirikiana na hazina ya taifa kuhakikisha rasilimali zinazoongezeka kwa mpango wa chanjo, kuhakikisha usambazaji thabiti wa chanjo.
Kenya ina changamoto ya chanjo kwa watoto baada ya serikali kukosa kununua chanjo za kutosha kwa muda uliofaa.
Nchi ilikosa kusambaza chanjo kwa mwaka mzima baada ya kushindwa kulipa deni la zaidi ya dola za Marekani milioni 15, ambazo ni sawa na shilingi bilioni mbili kwa muuzaji wa kimataifa.
Hatua hii inasemekana itaathiri takriban watoto wachanga milioni 1.6, idadi hii ya kina mama waja wazito na zaidi ya wasichana 750,000 chini ya umri wa miaka 10.