Hifadhi ya Kitaifa ya Meru nchini Kenya inakaribisha kuzaliwa kwa faru mweupe mpya, na kuongeza idadi ya wanyama hao.
Mwezi Agosti jumla ya ndama watatu wa faru weupe wamezaliwa.
Uzazi huo ulifanyika katika hifadhi hiyo, ambayo ni makazi ya faru weusi na weupe walio chini ya uangalizi wa saa 24 unaofanywa na walinzi.
Juhudi za uhifadhi za Shirika la Huduma ya Wanyamapori nchini Kenya zimeunda uwanja mzuri wa kuzaliana kwa vifaru katika hifadhi hiyo.
Kuzaliwa kwa kila ndama kunaashiria matumaini ya kuendelea kuwepo kwa faru weupe kwa wakati ujao, jambo linaloangazia maendeleo yanayofanywa katika uhifadhi wao.
Faru wengine weupe wa kipekee Kenya
Kenya inajivunia kuwa makazi ya faru wengine wawili wa aina yake waliobaki duniani.
Hawa ni faru weupe wa kaskazini au White Northern Rhinos. Faru hawa wanahifadhiwa katika Hifadhi ya Ol Pejeta iliyoko katika eneo la kati ya nchi.
Hawa ni jamii ndogo ya faru weupe, ambao walikuwa wakienea katika maeneo ya Uganda, Chad, Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Lakini pia kuna faru weupe wanaoitwa faru weupe wa Kusini au Southern Rhinos. Takwimu za mwaka 2023 zinaonyesha walikuwa 16,801.