Serikali ya Kenya imesema wananchi wa Comoro hawatahitaji tena visa kuingia Kenya.
"Ninakupa ahadi kwamba Kenya itasitisha hitaji la visa kwa watu wote walio na hati halali za kusafiri zinazotolewa na Muungano wa Comoro kuingia Kenya, kabla ya mwisho wa 2023," rais William Ruto amesema.
Ruto yupo Comoro kwa ajili ya sherehe za kuadhimisha miaka 48 ya siku ya Uhuru wa Muungano wa Comoros.
Siku ya Kitaifa ya Comoro au siku ya uhuru ya Comoros huadhimishwa Julai 6 kila mwaka.
Kenya pia imefungua nafasi za elimu kwa Comoro.
"Ili kuimarisha zaidi uhusiano wetu katika sekta ya Elimu, tunafanya mikakati ili kuruhusu wanafunzi kutoka Comoros kufuata masomo ya juu nchini Kenya na kulipa ada sawa na wanafunzi wa wetu." Ruto aliongezea.
Ruto alikaribishwa katika hafla hiyo kama mgeni mheshimiwa na rais Azali Assoumani kwa lengo kuu la kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.
Sikukuu hii ya kitaifa inaadhimisha siku ambayo nchi hiyo ilipata uhuru kutoka kwa Ufaransa mnamo 1975.
Comoro ni nchi ya kwanza ya visiwa kutwaa uenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) mapema mwaka huu, baada ya Rais wa Kenya William Ruto kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho.