Mtangazaji maarufu wa Kenya, Leonard Mambo Mbotela amefariki dunia.
Familia ya Mbotela ilitangaza kifo chake Ijumaa asubuhi jijini Nairobi.
Laonard Mambo Mbotela, maarufu wa kipindi cha redio , 'Je Huu ni Uungwana?' amefariki akiwa na miaka 85, ambapo zaidi ya miongo 6 ya maisha yake alifanyia kazi taifa katika fani ya utangazaji redioni na televisheni akisoma taarifa za habari, vipindi vya ucheshi na vya kutumbuiza pamoja na vipindi vya kuelimisha, Pia alikuwa mtangazaji mahiri wa Rais wakati wa sherehe rasmi za kitaifa.
Kipindi chake cha Je Huu ni Uungwana kilizinduliwa mwaka wa 1966, na kiliangazia nidhamu na ustaarabu katika jamii. Kipindi hiki kilipata umaarufu mkubwa na katika redio ya KBC kwa miongo kadhaa, na kukifanya kuwa moja ya vipindi vilivyodumu kwa muda mrefu katika historia ya utangazaji nchini Kenya.
![](https://images-cdn.trtworld.com/trtafricaswa/21532145_0-0-1279-928.jpeg)
Mapinduzi ya nchi
Leonard Mambo hata hivyo aliingia katika historia za Kenya kufuatia kuhusishwa katika jaribio la mapinduzi la 1982.
Leonard Mambo Mbotela anasimulia namna wanajeshi walimchukuwa nyumbani kwake alfajiri na kumshurutisha kutangaza katika redio ya taifa kuwa serikali imepinduliwa.
''Ilikuwa siku ya hatari sana. Wanajeshi walikuja kwangu nyumbani na kunichukuwa nikiwa na kikoi tu na fulana. Walisimama nyuma yangu na kunipa ukurasa wa kusoma...... Serikali imepinduliwa. Kila polisi aweke silaha chini na wafungwa wako huru...'' alisimulia Mbotela.
''Lakini muda mfupi baadaye jeshi la nchi kavu lilikomboa taifa na kurejesha utawala kwa Rais Moi. Pia nilitangaza redioni kuwa serikali imerudi kwa raia na rais ni Daniel Moi... nilifurahi kutangaza hilo kwa sababu amani ilirejea...'' aliendelea kusimulia Leonard Mambo Mbotela.
Kufuatia ujasiri wake huu, Leonard Mambo Mbotela alisifika kote nchini, alipendwa na kuheshimiwa na taifa.
Alipokea tuzo mbali mbali za kitaaluma pamoja na za kizalendo kutoka kwa marais mbali mbali zikiwemo pesa taslimu.
Mkufunzi, na Baba wa wengi
Aliwapa mafunzo watangazaji wengi na kukuza vipaji vyao katika tasnia ya utangazaji, yote kutokana na uongozi thabiti na uhodari wake katika uandishi wa habari.
Baada ya zaidi ya miongo 6 , Leonard mambo alistaafu ambapo aliendelea kuwepo mara kwa mara katika sherehe za kitaifa na mialiko rasmi ya tasnia ya uandishi wa habari.
Mbotela alizaliwa mwaka wa 1940 huko Freetown, Kaunti ya Mombasa
Ameacha mjane wake Alice Mwikali na watoto watatu.