Kenya yaambia wananchi wake Ethiopia kuwa makini wakati wa hali ya hatari

Kenya yaambia wananchi wake Ethiopia kuwa makini wakati wa hali ya hatari

Ethiopia imetangaza hali ya hatari ya miezi sita kwa eneo la Amhara
Wakenya nchini Ethiopia wameonywa kutoenda katika maeneo ambapo hakuna usalama kabisa  / Picha: AP Archive

Mnamo tarehe 4 Agosti 2023, serikali ya Ethiopia ilitangaza hali ya hatari katika mkoa wake wa Amhara.

Ethiopia imetangaza hali ya hatari ya miezi sita kwa eneo la Amhara na mkuu wa sheria nchini humo amesema, pia litatekelezwa katika maeneo mengine ya nchi kama itahitajika.

Hii ilifuatia ongezeko ya vita kati ya jeshi la serikali na vikundi vyenye silaha katika eneo hilo.

Serikali ya Kenya sasa imewaomba wananchi wa Kenya wanaoshi katika miji ambayo yameathiriwa na hali ya hatari kuwa makini wasivunje sheria mpya zilizowekwa na serikali ya Ethiopia.

Ubalozi wa Kenya nchini Ethiopia umewaonya waKenya dhidi ya kuzuru maeneo ambapo yameathiriwa moja kwa moja na hali ya hatari.

Kila mkenya nchini Ethiopia ameombwa kuzingatia sheria na kanuni zilizotolewa na serikali ya Ethiopia kuhusiana na hali ya hatari katika eneo la Amhara.

Wakenya wameonywa kutoenda katika maeneo ambapo hakuna usalama kabisa.

Ubalozi pia umewaomba kuwasiliana na maafisa wake kupitia njia za mawasiliano ambazo zimetolewa kwa mitandao.

Ukosefu wa usalama Amhara

Eneo la Amhara ndilo eneo la pili kwa ukubwa nchini Ethiopia. Mapigano yaliyozuka mapema wiki hii yamekuwa tishio kwa usalama.

Baraza la mawaziri lilisema kuwa hali ya hatari imekuwa muhimu kwa ajili ya kudhibiti mzozo ulioletwa na makundi ya silaha , ili kuhakikisha amani na usalama katika eneo hilo.

Amhara liliomba serikali kuu ya Ethiopia kuchukua hatua katika eneo hilo kwani hali ya usalama ilikuwa imezorota.

Serikali imesema kundi lenye silaha limekuwa likifanya ukiukwaji mkubwa kwa wakazi wa Amhara.

Maafisa wa serikali wanasema vikundi hivyo vimekuwa vikiwaibia wakazi wa eneo hilo na kuharibu vifaa vya kutoa huduma za umma pamoja na uhalifu mwingine.

TRT Afrika