Sehemu ya kutokea wasafiri ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya./Picha:Reuters

Na Brian Okoth

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya, umegeuka kuwa kaa la moto kwa Waziri wa Uchukuzi wa nchi hiyo, Kipchumba Murkomen.

Murkomen anatuhumiwa na baadhi ya Wakenya kwa kuutelekeza uwanja huo wa ndege, ambao unashika nafasi ya saba barani Afrika kwa kuwa na wingi wa abiria, kulingana na Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege duniani (ACI).

Wakenya hao wameoneshwa kuchukizwa na kukerwa na kukatika kwa mara kwa mara kwa umeme na mikanda ya mizigo ipigayo kelele, huku wakitaka jitihada za haraka za kunusuru hali hiyo.

Moja ya picha mjongeo katika mitandao wa X, zinaonesha abiria wakisubiri mizigo yao kutoka kwenye mikanda yenye kupiga kelele.

Hali huwa mbaya zaidi nyakati za mvua, huku baadhi ya picha hizo zikionesha kuvuja kwa paa la uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta.

Katika juhudi za kukabiliana na hali hiyo, serikali ya Kenya ilisema kuwa itaweka jenerat maalumu uwanjani hapo.

Kuhusu paa kuvuja, Murkomen aliwalaumu wahandisi waliojenga uwanja huo, enzi za utawala wa Rais Uhuru Kenyatta.

Hali huwa mbaya zaidi nyakati za mvua, huku baadhi ya picha hizo zikionesha kuvuja kwa paa la uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta./Picha: Reuters

"Tulipoingia madarakani, tulikuta viwanja vyetu wa ndege vikiwa katika hali mbaya sana, kuvuja kwa uwanja wa Jomo Kenyatta ni mfano tu," alisema Murkomen, Novemba 2023.

Murkomen, ambaye alizungumza katika kaunti ya Pwani ya Kwale nchini Kenya, alisema alimwagiza mwanakandarasi, aliyefanya ukarabati katika JKIA, kufanya ukarabati huo upya.

Katika mahojiano yake na kituo cha televisheni ya Citizen siku ya Jumatatu, Murkomen alisema matatizo ya uwanja huo yatataliwa kabla ya uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2027.

"Hadi kufikia kipindi cha uchaguzi ujao, tutakuwa tumepata kiwanja kipya na bora zaidi chenye kuleta ushindani mkubwa ," Murkomen alisema.

Kupitia ukurasa wake wa X siku ya Jumanne, Murkomen aliwataka baadhi ya Wakenya wanaooneshwa kuchukizwa na hali ya uwanja huo, akiwemo mwandishi mmoja maarufu, "kuacha kuongeza chumvi' na kuchafua taswira ya Kenya kimataifa."

Mnamo Aprili 2015, Kenya ilijenga seheku ya pili ya uwanja huo kwa gharama ya shilingi bilioni 1.7 za Kenya ($17.4 milioni) ili kupunguza msongamano, na sasa Murkomen anasema serikali iko katika harakati za kujenga sehemu nyingine.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Viwanja vya Ndege (ACI), JKIA ni uwanja wa ndege wa saba kwa shughuli nyingi zaidi barani Afrika, nyuma ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cairo wa Misri, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo wa Afrika Kusini na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cape Town, Uwanja wa Ndege wa Mohammed V wa Morocco, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hurghada wa Misri, na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Addis Ababa Bole ulioko Ethiopia.

Kulingana na takwimu hizo, uwanja huo ulihudumia abiria milioni 6.6 mwaka 2022.

Takriban abiria milioni 4.7 (asilimia 72) waliopitia JKIA walikuwa wasafiri wa kimataifa, jambo linaloonesha umuhimu wa kituo hicho kama kiunganishi muhimu cha Afrika Mashariki na sehemu nyingine za dunia.

JKIA ulifunguliwa kwa usafiri wa anga ya kibiashara mwaka wa 1958. Wakati huo, ukujulikana kama Uwanja wa Ndege wa Embakasi.

Mwaka 1978, uwanja huo ulibadili jina lake na kuitwa Uwanja wa Ndege wa Kenyatta, kama heshima kwa Baba wa Taifa la Kenya, Mzee Jomo Kenyatta.

TRT Afrika