Mahakama nchini Kenya imeamua kuwa ushuru wa nyumba uliozua utata ulioanzishwa na rais William Ruto haukuwa halali.
Ushuru wa asilimia 1.5 kutoka kwa mishahara ya Wakenya wote wanaolipa ushuru, iliyohitaji waajiri watoe hivyo pia, ulitiwa saini kuwa sheria mwezi Juni ili kufadhili mpango wa nyumba za bei nafuu.
Ushuru huo ulikuwa kati ya mapendekezo ya mabadiliko katika sheria ya fedha ya nchi.
Kamati ya majaji watatu katika Mahakama Kuu jijini Nairobi ilisema Jumanne kuwa hakukuwa na mfumo kamili wa kisheria wa kuanzishwa kwa ushuru huo.
Mahakama iliona kuwa sio haki kutoza ushuru wa nyumba wa 1.5% kwa Wakenya wanaopokea mishahara pekee.
Lakini sasa Serikali imefanya marekebisho kwa vipengele vilivyokuwa na utata na kurejesha mswada huo bungeni kujadiliwa upya.
Nani ataokota Ushuru?
Moja ya sababu zilizofanya Ushuru wa Nyumba kutupiliwa mbali na mahakama ya majaji watatu ilikuwa ni suala la nani anakusanya ushuru.
" Hili ni suala kubwa sana kwa sababu ya vipande vya sheria pamoja na idadi ya ofisi zinazoingiliana katika kufikia ukiukaji wa katiba," anaelezea Julian Amboko mtaalamu wa maswala ya biashara, katika akaunti yake ya X.
Sheria hiyo ilipendekeza kuwa ushuru ukusanywe na Mamlaka ya Mapato nchini Kenya Revenue Authority, KRA. Idhini hii ilipatiwa KRA na baraza la mawaziri Agosti mwaka huu.
Swala hili lilipingwa na majaji ambao walidai katika sheria ya KRA, Ushuru wa Nyumba si mojawapo ya maeneo ya mapato. Pia mahakama ilidai kuwa chini ya sheria hiyo, Waziri aliye na mamlaka ya kuipa KRA idhini ni waziri wa hazina bali si waziri wa ardhi kama ilivyokuwa.
Katika mswada huu mpya amabo umeletwa tena bungeni serikali imerekebisha kuwa "Katibu wa Baraza la Mawaziri" ndani ya Sheria atakuwa ndiye anayesimamia nyumba za bei nafuu.
Pia imeelezea kua mtoza ushuru atakuwa kamishna mkuu wa KRA ama yeyote atakayeteuliwa na Kamishna mkuu wa KRA.
Nani atalipia Ushuru?
Swala lingine mahakama ilitaja ni kile ambacho majaji walisema ni ubaguzi wa ulipaji ushuru hii, ikidai haikuwa na kanuni za usawa katika ushuru.
Ingelipwa na wale tu mabao walikuwa wameajiriwa rasmi huku ikiondoa wale ambao hawajaajiriwa asmi hivyo hawana vyeti vya kuonyesha mapato yao, (hawana pay slip) ambayo iko kwa urahisi ndani ya rada ya KRA.
"Labda hapo ndipo labda mfumo wa ushuru wa E tims unaweza kuingilia," Amoko anasema hapo kwa X,
Mfumo huu unatumika na wafanyabiashara na hivyo inaweza kupata ushuru kutoka kwa wale ambao wawapo katika mifumo rasmi ya mshahara.
Uhusiano na mfuko wa nyumba.
Suala lingine ambalo ambalo lilipingwa na mahakama ni mfumo wa kisheria unaozingatia Ushuru wa Nyumba na ukweli kwamba Sehemu ya 84 ya Sheria ya Fedha ya 2023 haionyeshi uhusiano wowote kati ya ushuru wa nyumba na Mfuko wa Maendeleo ya Nyumba (NHDF).
Katika marekebisho ya mswada uliowakilishwa bungeni ,inaonesha serikali inaanzisha hazina ya nyumba ya bei nafuu na inabadilisha muundo wa shirika pamoja na usimamizi na uendeshaji wa hazina hiyo.
" Hii pia inashughulikia suala la jinsi mapato ya Ushuru wa Nyumba yatasimamiwa mara tu yatakapokusanywa," Amboko anaongezea.