Kaimu inspekta jenerali wa polisi nchini Kenya ameripotiwa kukosa kuheshimu mahakama kwa kukosa kufika mbele ya hakimu mara sita.
Gilbert Masengeli amemtuma Naibu Inspekta Jenerali wa polisi, Eliud Langat kwa niaba yake akisema anahusika katika operesheni ya usalama katika Kaunti ya Wajir.
Masengeli alitarajiwa kufika mahakamani Jumatatu kama alivyoamuru Jaji Lawrence Mugambi la sivyo atakabiliwa na adhabu ya kupuuza wito wa mahakama.
Masengeli alitakiwa kuelezea mahakama kuhusu madai ya kutekwa nyara kwa ndugu wawili na mwanaharakati, ikiwa watatu hao wametoweka kwa wiki mbili.
Kaimu IG alikuwa ameagizwa kufika mbele ya hakimu ana kwa ana kueleza ni kwa nini wanaume hao watatu waliotekwa nyara huko Kitengela, Nairobi hawajaachiliwa.
Ndugu wawili Jamil Longton, Aslam Longton, na mwanaharakati Brian Njagi inaripotiwa walichukuliwa na watu waliovalia suti waliodai kuwa maafisa wa polisi kutoka Nairobi lakini hawakutoa sababu ya kuwakamata.
Aliyekuwa Rais wa Jumuiya ya wanasheria Kenya Nelson Havi alimwomba Jaji Lawrence Mugambi amfunge Masengeli katika jela ya kiraia kwa muda wa miezi sita kwa kukaidi maagizo ya mahakama. "Mienendo ya Insekta Jenerali lazima ishughulikiwe na mahakama na kwa ukali iwezekanavyo," alisema.
Wakili mkuu wa serikali Charles Mutinda kwa upande mwingine aliambia mahakama hakuna msingi wa kaimu IG kupatikana na hatia.
“Tumetoa maelezo na kufafanua zaidi na hata kumleta ofisa mwengine mkuu kufika mahakamani na kutoa maelezo,” alisema kuwa Masengeli yuko Wajir na hakuweza kufika mahakamani.