Maandamano hayo yalihamasishwa kupitia mitandao ya kijamii./Picha: AA

Waandamanaji nchini Kenya wameendeleza maandamano mengine siku ya Alhamisi kama ishara ya kupinga muswada wa fedha na ongezeko la kodi linalotishia kupanda kwa gharama za maisha nchini humo.

Hata hivyo, serikali ya nchi hiyo bado itaendelea kutekeleza ongezeko la kodi ikisema hatua hiyo inalenga kutunisha hazina yake na kupunguza utegemezi wa ukopaji kutoka nje.

Waandamanaji hao wamenuia kuendelea na maandamano hayo nchi nzima, pamoja na maeneo ya Mombasa na Kisumu ambayo ni himaya za upinzani.

Barabara zafungwa

"Wanapaswa kukataa muswada ule sio kuuhariri," Sarah Njoroge aliiambia AFP. "Wanadhani kuwa tutapaza sauti zetu kwenye mitandao ya kijamii tu na kuwa tutachoka."

Mamlaka zilifunga barabara karibu na jengo la bunge mjini Nairobi, huku kukiwa na idadi kubwa ya walinda usalama, ambapo wabunge wanatarajiwa kuanza kujadili muswada huo siku ya Jumatano.

Waandamanaji mjini Nairobi wamesisitiza kuwa watatembea kuelekea kwenye eneo la bunge, ambalo ni lazima lipitishe toleo la mwisho la muswada huo kabla ya Juni 30.

Chanzo za bunge kiliiambia AFP kuwa kura kwa mapendekezo ya muswada huo inatarajiwa kupigwa Juni 27.

Upungufu

Kodi hizo zilitarajiwa kuongeza dola bilioni 2.7 ambayo ni sawa ya asilimia 1.9 ya pato la taifa, na kupunguza upungufu wa bajeti kutoka asilimia 5.7 mpaka 3.3 ya pato la taifa.

Siku ya Jumanne, ofisi ya Rais ilitangaza kuondoa baadhi ya kodi zilizopendekezwa kwenye manunuzi ya mikate, umiliki wa magari pamoja na huduma za miamala ya kifedha, jambo lililoibua onyo kutoka hazina kuhusu upungufu wa bilioni 200 kutokana na maamuzi hayo.

Kwa sasa, serikali ya Kenya imelenga ongezeko kwenye bei ya mafuta na kodi za mauzo ya nje kuziba ombwe linalotokana na mabadiliko, hatua ambayo wakosoaji wanasema itasababisha ugumu wa maisha zaidi huku nchi hiyo ikikumbana na viwango vikubwa vya mfumuko wa bei.

Dharau

Takribani watu 335 walikamatwa wakati wa maandamano hayo, kulingana na taasisi za haki za binadamu ikiwemo Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR) na Amnesty Kenya.

"Tumebadili mbinu. Leo tutavaa mavazi tufauti ili kuepusha watu kukamatwa," alisema mmoja wa waandamanaji.

Kenya ni mojawapo ya nchi zenye uchumi unaoendelea katika ukanda wa Afrika Mashariki. Hata hivyo, theluthi moja ya watu wake milioni 51.5 wanaishi katika umaskini.

TRT Afrika