Marekani inajadili ni msaada gani itatoa kwa kikosi cha kimataifa kinachoongozwa na Kenya kinachoenda kusaidia polisi nchini Haiti kupambana na magenge yenye silaha huku kukiwa na hali mbaya zaidi ya kibinadamu huko.
''Ahadi ya Kenya ni kupeleka polisi 1,000 kusaidia kutoa mafunzo na kusaidia polisi wa Haiti kurejesha hali ya kawaida nchini na kulinda mitambo ya kimkakati.'' Taarifa kutoka wizara ya mambo ya nje ya Kenya ilisema wiki iliyopita.
Naibu Katibu Msaidizi wa Mambo ya Nje wa Masuala ya Caribbean na Haiti Barbara Feinstein aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa kwamba michango ya Marekani itategemea matokeo ya tathmini ya Kenya inayotarajiwa kufanyika katika mji mkuu wa Haiti wiki zijazo.
Marekani imesema iko tayari kuwasilisha muswada katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha kikosi kama hicho.
"Tutakuwa tukifanya kila tuwezalo kuunga mkono mchakato huo na kuhakikisha kupitishwa kwa azimio hilo haraka," Feinstein alisema.
Alisema Marekani itatafuta michango kama vile wafanyakazi, vifaa, mafunzo, ufadhili au msaada mwingine kutoka kwa nchi kote ulimwenguni.
Mapendekezo kutoka kwa ripoti ya Umoja wa Mataifa inayotarajiwa Agosti 15 yana uwezekano wa kuchangia jinsi kikosi hicho kingeonekana, alisema.
Serikali ya Haiti iliomba msaada wa kimataifa wa usalama mwaka jana na Umoja wa Mataifa umerudia mara kwa mara kuunga mkono Haiti ipate usaidizi wa usalama.
Lakini hakuna nchi ambayo imekuwa tayari kuongoza juhudi kama hizo hadi Kenya iliposema kuwa iko tayari kufanya hivyo wiki iliyopita na kwa kujitolea kutuma maafisa 1,000.
Nchi nyingi zimekua zikihofia kujihusisha katika nchi hiyo iliyo na uongozi wa muda ambao haukuchaguliwa kwa kura na kuwepo kwa historia ya nchi za kigeni nyingi kuingilia masuala ya Haiti ,
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipongeza hatua ya Kenya kuridhia kuongoza kikosi cha kimataifa kusaidia polisi wa Haiti kupambana na ghasia za magenge na kuhimiza nchi nyingine - hasa kutoka eneo la Haiti - kujiunga na jitihada.