Katika sehemu zote nchini , usafiri kwa kutumia huduma ya bodaboda imekuwa kitu cha kawaida.
Kwa maeneo mengine ya makazi, hii ndiyo njia pekee ya watu kufika makwao.
Lakini pia bodaboda wamekuwa mbinu mbadala ya usafiri ikiwa mtu ana haraka na hataki kukwama katika changamoto ya msafara wa magari barabarani.
Wafanya biashara pia wanatumia bodaboda kuwachukuliwa wateja wao bidhaa za aina mbali mbali.
Lakini sekta hii bado haijarasimishwa , ikiwa kuna watu wengine ambao wanamiliki pikipiki zao wenyewe, wengine wanakodisha kwa masaa machache na wengine ili kujipatia mapato.
Rais William Ruto amesema serikali inataka kuweka mchakato wa kurasimisha sekta hii inayobuni nafasi za kazi milioni 1.5 na kuzalisha zaidi ya dola milioni mbili kila mwaka.
"Tutashirikiana na washikadau wote kuhakikisha mafunzo na utoaji wa leseni kwa waendesha boda boda usiyozidi dola 18," rais William Ruto alisema.
Programu ya serikali ya kuwainua Boda Boda
Ruto alisema kurasimisha sekta hiyo pia kutarahisisha upatikanaji wa mikopo nafuu kupitia mchakato wa "hustler fund".
Alibainisha kuwa awamu ya awali ya mpango huo utafundisha waendeshaji 200,000 waliochaguliwa kutoka kaunti zote 47.
Mafunzo hayo yatahusu usalama barabarani, kanuni za barabarani, usimamizi wa ajali, ujasiriamali na usimamizi wa fedha.
Rais alisema serikali inapunguza ushuru wa sehemu za pikipiki za umeme ili kupunguza gharama ya bidhaa ya mwisho na kuhimiza matumizi yake.
"Kwa kutumia pikipiki ya umeme, utaokoa hadi asilimia 68 ya gharama ya matumizi kwa pikipiki za umeme na kuokoa hadi asilimia 30 ya gharama za kuhudumia," alisema.