Baraza la Mitihani la Taifa la Kenya, KNEC limetangaza kuwa litaanzisha mitihani ya mwisho ya sekondari katikati ya mwaka, mbali na ile ya mwisho wa mwaka.
"KNEC itaanzisha mfululizo wa katikati ya mwaka wa KCSE utakaosimamiwa Julai kila mwaka," Waziri wa Elimu Julius Migos amesema huku akitangaza matokeo ya mitihani ya 2024.
"Mtihani huo utalenga watahiniwa wanaotaka kurudia mitihani au wale ambao wanaweza kukosa kuhudhuria mitihani kwa sababu ya ugonjwa au ugumu usiotarajiwa," ameongezea.
Waziri amesema wanafunzi wa uzeeni pia wanaweza kuamua kujisajili kwa mitihani ya kati kati ya mwaka.
Matokeo ya mitihani ya mwaka 2024
Wizara ya Elimu imetangaza matokeo ya mitihani ya sekondari ya 2024.
"Leo tunatoa matokeo ya KCSE 2024 kwa watahiniwa 962,512, ambao wote tumewaidhinisha kujiunga na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu ili kusomea taaluma walizochagua," Waziri Migos amesema.
Kwa mara ya kwanza idadi ya wanafunzi wa kike imezidi ya wanafunzi wa kiume. Jumla ya 482, 202 wa kike walifanya mitihani.
Wanafunzi 1,693 walipata alama ya juu kabisa ya A, huku 246, 391 wakipata alama za C+ na juu na hapo kupata uwezo wa moja kwa moja wa kuingia katika vyuo vikuu.
Matokeo ya watahiniwa 840 yalifutwa baada ya kuhusika katika udanganyifu wa mitihani. Matokeo ya wengine 2,829 hayajatoka, huku walimu 91 wakingoja kuchukuliwa hatua ya kisheria.
Kenya imebadilisha mfumo wa elimu. Badala ya kusoma miaka nane elimu ya msingi, minne sekondari na minne chuo kikuu, hivi sasa wanafunzi wanasoma miaka sita shule za msingi, miaka mitatu sekondari ya chini, miaka mitatu sekondari ya kawaida na miaka mitatu chuo kikuu.
"Ningependa kuwakumbusha umma kwamba mtihani wa mwisho wa KCSE utafanywa 2027. Mtu yeyote anayetaka kurudia kikamilifu au kwa kiasi anapaswa kutumia fursa iliyosalia kufanya hivyo,” Dkt, David Njegere, Mkurugenzi Mtendaji wa KNEC amesema.