Wanajeshi wa Uingereza wakiwa katika mafunzo ndani ya kambi ya jeshi la Uingereza huko Laikipia. Picha/ Reuters

Kenya siku ya Jumanne inatazamiwa kuanzisha vikao vya hadharani kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu na matumizi mabaya ya mamlaka na wanajeshi wa Uingereza waliokita kambi Kenya.

Kitengo cha Mafunzo ya Jeshi la Uingereza nchini Kenya (BATUK) ni tegemeo la kiuchumi kwa wengi katika mji wa kati wa Nanyuki, lakini askari walioko humo pia wameshutumiwa kwa kutenda makosa yakiwemo mauaji.

Katika kisa hatari cha mwaka wa 2012, mwili wa mama mdogo Mkenya ulipatikana kwenye tanki la maji taka, huko Nanyuki ambapo mara ya mwisho alionekana akiwa pamoja na mwanajeshi wa Uingereza.

Familia ya Agnes Wanjiru iliwasilisha kesi nchini Kenya kuhusu kifo cha msichana huyo mwenye umri wa miaka 21, lakini kesi hiyo imekua ikipelekwa taratibu, ikiahirishwa mara kwa mara. Kesi hiyo sasa inatazamiwa kusikizwa Julai 10, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.

'Ukiukaji wa maadili'

Bunge la Kenya lilitangaza wiki jana kuwa litafanya mikutano minne ya hadhara, ikiwa ni pamoja na mmoja mjini Nanyuki, kuhusu madai ya dhuluma na wanajeshi wa Uingereza walioko nchini humo.

Vikao hivyo vitakavyo fanyika kati ya Jumanne na Alhamisi wiki hii "vitachunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kutendewa vibaya, kuteswa, kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria, mauaji," duru iliyotolewa na baraza la chini la bunge ilisema.

Vikao hivyo pia vitachunguza "madai ya ukiukaji wa kimaadili unaohusiana na utovu wa maadili, ikiwa ni pamoja na rushwa, ulaghai, ubaguzi, matumizi mabaya ya mamlaka na tabia nyengine zisizo za kimaadili."

London na Nairobi zimekuwa katika mzozo kuhusu suala la mamlaka ya wanajeshi wa Uingereza wanaovunja sheria za Kenya, huku serikali ya Uingereza ikisema hapo awali kwamba haikukubali mamlaka ya mahakama ya Kenya kuchunguza kifo cha Wanjiru.

Alipoulizwa kuhusu vikao vya wiki hii, msemaji wa Ubalozi wa Uingereza aliiambia AFP: "Ubalozi wa Uingereza mjini Nairobi na BATUK wanakusudia kushirikiana na uchunguzi huo.

"Ushirikiano wa ulinzi wa Uingereza na Kenya ni mojawapo ya nguvu kuu za uhusiano wetu, na mafunzo na operesheni zetu za pamoja na Wanajeshi wa Ulinzi wa Kenya zinawaweka watu wa Kenya na Uingereza salama."

Kudai haki

Siku ya Alhamisi, ujumbe wa Uingereza ulisema Kamishna Mkuu Neil Wigan, alikutana na familia ya Wanjiru, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikidai haki kuhusu mauaji yake.

"Mkutano huo ulitoa fursa kwa Kamishna Mkuu kusikiliza familia na kutoa rambirambi zake. Kamishna Mkuu pia alikariri kujitolea kwa Uingereza kushirikiana kikamilifu na uchunguzi wa Kenya kuhusu kifo cha Bi Wanjiru," ilisema.

Mnamo Oktoba 2021, gazeti la The Sunday Times la Uingereza liliripoti kwamba mwanajeshi mmoja alikiri kwa wenzake kumuua Wanjiru na kuwaonyesha mwili wake.

Ripoti hiyo ilidai kuwa wakuu wa jeshi walifahamishwa kuhusu mauaji hayo, lakini hakuna hatua zaidi zilizochukuliwa.

Uchunguzi ulifunguliwa mnamo 2019 lakini hakuna matokeo ambayo yametolewa kwa umma.

Polisi wa Kenya walitangaza kuwa uchunguzi huo utafunguliwa tena baada ya ufichuzi wa gazeti la Sunday Times.

Familia ya Wanjiru imeshirikiana na polisi wa Kenya na maafisa wa sheria na kisiasa kufungua kesi mahakamani dhidi ya jeshi la Uingereza nchini Kenya.

TRT Afrika