Paul Mackenzie kiongozi wa ibada ya njaa alikuwa anakula huku akiwashawishi wafuasi wake wajinyime chakula

Tangu Aprili mwaka huu serikali ya Kenya inaendelea kufanya msako wa wananchi katika msitu wa Shakahola, pwani mwa Kenya.

Paul Mackenzie kiongozi wa ibada ya njaa, aliwashawishi mamia ya watu kuhama makwao na kuishi katika msitu huo na wakijinyima chakula akidai kuwa wangemwona Yesu Kristu.

Waziri wa Mambo ya Ndani na utawala wa kitaifa nchini Kenya, Kithure Kindiki alitembelea makazi ya Paul Mackenzie katika msitu huo wa Shakahola.

"Katika baadhi ya makazi ndani yake kwa msitu wa Shakahola, tulipata ratiba ya chakula iliyowekwa vizuri kama ile ya hoteli kubwa," waziri Kindiki ameelezea, " " Mackenzie na maskauti wake walikuwa wanakula mlo kamili; kifungua kinywa, chakula cha mchana, na chakula cha jioni karibu na watu wenye njaa na wanaokufa."'

Watu 240 wameripotiwa kufa baada ya kufuata ibada hii, wengi wao walifukuliwa kutoka makaburi iliyopatikana katika sehemu tofauti katika msitu huo wenye ukubwa wa ekari 800.

Kindiki anaelezea kuwa uchunguzi umevumbua kuwa Mackenzie alikuwa ameajiri vijana wenye silaha kama walinzi wa kuwaangalia wafuasi wake na kuhakikisha wanajinyima chakula hadi kufa .

Ratiba ya Chakula Shakahola | Picha: Wizara ya Mambo ya Ndani

"Inasemekana wale wafuasi ambao walibadili nia na kutaka kuwacha kunjinyima chakula waliuawa kwa kunyongwa au kugongwa na vifaa," Kindiki ameongezea.

Awamu ya pili ya uchunguzi wa uchunguzi wa miili 129 imeanza katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi.

Msako wa watu zaidi pia unaendelea, lakini ufukuaji wa miili na makaburi utaendelea baada ya uchunguzi wa miili iliyopatikana kukamilika.

"Gaidi huyu wa Mackenzie alikuwa anafanya makusudi katika kila alichokuwa akifanya. Aliepuka matumizi ya teknolojia...baadhi ya makaburi ya halaiki yalifunikwa na uoto, na ndiyo maana maafisa wetu wanalazimika kutafuta makaburi hayo," waziri amesema.

Serikali ya Kenya inasema haitaingilia uhuru wa kuabudu lakini itawasaka wahalifu wanaojificha katika mashirika ya kidini na kutumia maandiko matakatifu kwa nia ya kuwapotosha wafuasi wao.

Wizara hiyo inayoongoza oparesheni ya kuwasaka watu katika msitu wa shakahola inasema , miili mingi iliyofukuliwa ilikuwa ya watu waliouawa na kuzikwa baada ya Machi 22, 2023.

Hii ni baada ya Mackenzie kuachiliwa na mahakama kwa dhamana ya takribani dola 100. Alikuwa amekamatwa baada ya kuhusishwa vifo vya watoto wawili ambao walisemekana walikufa kwa njaa.